Uturuki na Russia zatupilia mbali sarafu ya dola katika biashara
Uturuki na Russia zimetia saini mapatano ya kutupilia mbali sarafu ya dola katika mabadilishano ya kibiashara baina yao.
Wizara ya Fedha ya Russia imetangaza kuwa, kwa mujibu wa mapatano yaliyotiwa saini, sarafu za Ruble ya Russia na Lira ya Uturuki zitatumika katika malipo na miamala ya kifedha baina ya nchi mbili.
Kwa mujibu wa mapatano hayo, nchi hizo mbili zitaanza kutekeleza hatua kwa hatua mpango huo wa kutumia sarafu za kitaifa katika biashara ya pande mbili. Biashara baina ya nchi hizo iliongezeka kwa silimia 16 mwaka jana na kufika dola bilioni 25.5.
Aidha mapatano hayo yanalenga kuunganisha banki za Uturuki na mfumo wa kimataifa wa mabadilishano ya kifedha wa Russia ambao umechukua sehemu ya ule wa kimataifa wa SWIFT unaosimamiwa na Marekani.

Aidha banki za Uturuki zitawezeshwa kutumia mfumo wa kadi za benki za MIR za Russia ambazo zinachukua nafasi ya zile kadi za benki za Kimarekani za VISA na MasterCard. Mapatano hayo ni katika mkakati wa nchi hizo mbili kuacha kutegemea sarafu ya dola ya Marekani.
Hivi karibuni Gavana wa Banki Kuu ya Iran Abdolnaser Hemmati alitangaza kuwa Uturuki, Iran na Russia zimeafikiana kuacha kutumia sarafu ya Marekani na badala yake kutumia za ndani katika biashara kati ya mataifa hayo matatu.