Iran yalaani shambulizi la kigaidi lililoua makumi msikitini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56720-iran_yalaani_shambulizi_la_kigaidi_lililoua_makumi_msikitini_afghanistan
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali shambulizi la kigaidi lilioua makumi ya watu ndani ya msikiti katika mkoa wa Nangarhar mashariki mwa Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 19, 2019 08:59 UTC
  • Iran yalaani shambulizi la kigaidi lililoua makumi msikitini Afghanistan

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali shambulizi la kigaidi lilioua makumi ya watu ndani ya msikiti katika mkoa wa Nangarhar mashariki mwa Afghanistan.

Msemaji wa wizara hiyo, Abbas Mousavi sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga, serikali na taifa la Afghanistan kufuatia shambulizi hilo la jana Ijumaa, amesema kitendo hicho cha kuwalenga waumini ambao hawana ulinzi tena ndani ya Nyumba ya Allah ni ukatili wa kupindukia.

Amesema, "Kitendo hicho cha ugaidi dhidi ya waumini wasiokuwa na ulinzi kwa mara nyingine kimeonesha sura halisi ya ugaidi na lengo la magaidi la kupanda mbegu za chuki na uhasama miongoni mwa Waislamu."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebanisha kuwa, shambulizi hilo limeongeza mafuta kwenye moto wa ukosefu wa usalama na uthabiti katika nchi hiyo jirani ya Kiislamu.

Miili ya maiti ikiwa ndani ya msikiti ulioshambuliwa nchini Afghanistan

Watu wasiopungua 62 waliuawa na wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa katika miripuko kadhaa ya mabomu iliyotokea jana wakati wa Sala ya Ijumaa ndani ya msikiti katika mkoa wa Nangarhar mashariki mwa Afghanistan.

Wakati huohuo, Umoja wa Mataifa umetoa taarifa ya kulaani hujuma hizo za kikatili dhidi ya raia wasio na hatia nchini Afghanistan.