Rais Putin wa Russia ataka kuhitimishwa mgogoro wa Libya
(last modified Thu, 19 Dec 2019 12:55:58 GMT )
Dec 19, 2019 12:55 UTC
  • Rais Putin wa Russia ataka kuhitimishwa mgogoro wa Libya

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema angependa kuona mgogoro wa Libya unapatiwa ufumbuzi na mazungumzo baina ya pande mbili hasimu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika yanaanza.

Putin amesema hayo leo Alkhamisi katika kikao cha kila mwaka na waandishi wa habari mjini Moscow na kuongeza kuwa, "Tutajadili kadhia ya Libya na ujumbe wa Uturuki nchini Russia ndani ya siku chache zijazo."

Moscow na Ankara zimekuwa zikiunga mkono pande hasimu kwenye mgogoro wa Libya ulioanza mwaka 2014.

Mgogoro wa sasa wa Libya umesababisha nchi kadhaa kuvutana na hata kupelekea kuibuka mikwaruzano ya kidiplomasia. 

Haftar alianzisha mashambulizi dhidi ya Tripoli siku chache baada ya kuonana na Mfalme wa Saudia

Hivi karibuni, Libya ilitangaza habari ya kufunga ubalozi wake katika mji mkuu wa Misri Cairo, kutokana na kile kilichotajwa kuwa sababu za kiusalama.

Tangu jenerali muasi Khalifa Haftar aanzishe mashambulizi dhidi ya mji wa Tripoli Aprili mwaka huu kwa msaada wa kila upande wa Saudia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na baadhi ya nchi za Magharibi, hadi sasa amesababisha zaidi ya watu 1090 kuuawa na wengine wasiopungua 5700 kujeruhiwa.