ICJ: Myanmar imewasababishia Waislamu wa Rihongya maumivu yasiyofidika
https://parstoday.ir/sw/news/world-i58705-icj_myanmar_imewasababishia_waislamu_wa_rihongya_maumivu_yasiyofidika
Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) imeitaka serikali ya Myanmar kuchukua hatua za dharura za kuzuia mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Rohingya, ikisisitiza kuwa Warohingya hao wamesababishiwa machungu na maumivu yasiyoweza kufutika au kurekebishika.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 24, 2020 02:53 UTC
  • ICJ: Myanmar imewasababishia Waislamu wa Rihongya maumivu yasiyofidika

Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) imeitaka serikali ya Myanmar kuchukua hatua za dharura za kuzuia mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Rohingya, ikisisitiza kuwa Warohingya hao wamesababishiwa machungu na maumivu yasiyoweza kufutika au kurekebishika.

Akisoma agizo la majaji wote 17 wa mahakama hiyo iliyoko The Hague nchini Uholanzi jana Alkhamisi, Rais wa ICJ, Abdulaqawi Ahmed Yusuf, amesema, "Mynamar imesababisha hasara isiyofidika kwa kukanyaga haki za Warohingya."

Novemba mwaka uliopita, Gambia iliwasilisha faili la kesi ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Warohingya katika mahakama hiyo ya juu ya Umoja wa Mataifa iliyoko The Hague.

Gambia ilisema imechukua hatua hiyo ili kutafuta haki na kuhakikisha wahusika wa mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Myanmar dhidi ya Warohingya katika mkoa wa Rakhine wanabebeshwa dhima.

Watoto wa Warohingya wanaofanyiwa ukatili na jeshi la Myanmar

Faili hilo limeanza kusikilizwa na ICJ katika hali ambayo, wiki chache zilizopita, maafisa wa Umoja wa Mataifa walitoa wito wa kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ili kushughulikia jinai zinazofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine nchini humo.

Maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameuliwa, laki nane wamejeruhiwa na wengine wapatao milioni moja wamelazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh ili kunusuru maisha yao, baada ya jeshi na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka kuanzisha mauaji ya kinyama Agosti 25 mwaka 2017.