Mgogoro wa elimu waishtua UN, watoto milioni 258 hawaendi shule
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuna mgogoro mkubwa wa elimu duniani hivi sasa, na kwamba watoto zaidi ya milioni 258 walio chini ya umri wa miaka 17 hawaendi shule.
Amina Mohammed alisema hayo jana Ijumaa katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa mnasaba wa Siku ya Elimu Duniani na kuongeza kuwa, ni asilimia 49 tu ya wanafunzi wanaofanikiwa kukamilisha masomo ya shule za sekondari.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa UN ameeleza bayana kuwa, watu wazima milioni 770 kote duniani, aghalabu yao wakiwa ni wanawake hawajui kusoma wala kuandika.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya elimu, Gordon Brown ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza akizungumza katika kikao hicho cha jana mjini New York alisema kuwa, "inaendelea kunishtua namna watoto milioni 400 wenye umri kati ya miaka 11 na 12 wanakatiza masomo kabisa, na milioni 800 wanakamilisha mfumo wa elimu bila kuambulia chochote."
Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limeonya kuwa, iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa mamilioni ya watoto hawatakuwa na uwezo wa kwenda shule na kupata elimu, na kwamba mgogoro huo utasababisha kutofikiwa Malengo ya Ustawi Endelevu yaliyoainishwa na jamii ya kimataifa hadi kufikia mwaka 2030.