Msimamo mkali wa Boris Johnson katika mazungumzo na Umoja wa Ulaya
Baada ya Uingereza kujitoa rasmi katika Umoja wa Ulaya tarehe 31 ya mwezi uliopita wa Januari, filihahi suala muhimu yaani mazungumzo baina ya London na Brussels kuhusiana na utambulisho na muundo wa uhusiano wa pande mbili katika kipindi cha baada ya Brexit ndilo linalojadiliwa sasa.
Kwa kuzingatia kipindi cha mpito cha miezi 11 ambacho kwa uchache kinatarajiwa kufikia tamati tarehe 31 Disemba mwaka huu, kuanzia sasa London imechukua msimamo mkali mkabala wa Umoja wa Ulaya.
Katika uwanja huo, akihutubia Jumatatu iliyopita Boris Johnson Waziri Mkuu wa Uingereza alitangaza masharti yake kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Umoja wa Ulaya na kusisitiza kwamba, hata kama hataweza kufikia makubaliano ya kibiashara na umoja huo kama anavyotaka, pamoja na hayo, Uingereza itapiga hatua za kimaendeleo.
Matini ya hotuba ya Waziri Mkuu wa Uingereza iliyosambazwa na ofisi yake inaonyesha kuwa, Johnson amesisitiza kwamba: Hakuna haja ya kuweko makubaliano ya biashara huru ambayo yatajumuisha humo kukubali kanuni za Umoja wa Ulaya katika uga wa kisiasa, ruzuku, huduma za kijamii, mazingira na mfano wa hayo. Bali inatosha tu Umoja wa Ulaya ukubali kanuni za Uingereza.

Boris Johnson sambamba na kuahidi kwamba, atalinda na kuhifadhi viwango vya juu kabisa ameunasihi Umoja wa Ulaya kwamba, upendekeze makubaliano ya biashara huru yanayoshabihiana na yale ya Canada ambapo kwa mujibu wake, serikali ya Ottawa haifuati sheria za Umoja wa Ulaya. Johnson anasema kuwa:
Umoja wa Ulaya una hiari ya kukubali au kukataa matakwa yetu. Suala lililopo hapa ni kwamba, je sisi tutafikia makubaliano ya uhusiano wa kibiashara na Umoja wa Ulaya kama yale yaliyofikiwa na umoja huo na Canada au tutakuwa na uhusiano na EU kama ule ulionao umoja huo na Australia?
Filihali sehemu kubwa ya makubaliano ya biashara ya Umoja wa Ulaya na Australia yamejengeka juu ya msingi wa sheria za Shirika la Biashara Duniani (WTO), pamoja na kuwa kuna makubaliano maalumu katika baadhi ya bidhaa maalumu. Pamoja na hayo, Australia ipo katika mwenendo wa mazungumzo na Umoja wa Ulaya kuhusiana na makubaliano ya kibiashara.

Hili ni jambo ambalo limetiliwa mkazo pia na Dominic Raab, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza. Raab amesema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Uingereza haifuatilii suala la kuoainisha kanuni zake na zile za Umoja wa Ulaya. Sisi tuna sheria zetu, hivyo basi hatutaki tuendane sana na Umoja wa Ulaya pamoja na kanuni zao. Sisi tunataka kuwa na ushirikiano na tunataraji Umoja wa Ulaya nao utafuatilia ahadi zake kuhusiana na kuweko makubaliano huru ya kibiashara yenye mtindo kama ule wa Canada.
Licha ya kutangazwa matarajio na matakwa ya serikali ya kihafidhina ya Uingereza kwa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo yajayo, nchini Uingereza kwenyewe kuna upinzani dhidi ya utendaji wa sasa wa serikali katika uwanja huo.
Keir Starmer, Waziri Kivuli wa Brexit kutoka katika chama cha upinzani cha Leba ameonya kuwa, siasa za Boris Johnson zitaudhuru uchumi wa Uingereza. Starmer amesema: Boris Johnson ama hadiriki au kwake si jambo muhimu kwamba, siasa zake zinailetea madhara Uingereza.

Katika radiamali dhidi ya msimamo na matakwa ya London ya kuamiliwa nchi hiyo kama Canada, viongozi wa Umoja wa Ulaya wametahadharisha kwamba, Canada imefanikiwa kufikia katika hali ya sasa ya biashara na Umoja wa Ulaya kutokana na kutabikisha sehemu kubwa ya sheria zake na kanuni za umoja huo.
Umoja wa Ulaya umeitahadharisha Uingereza mara nyingi kwamba, kiwango cha kufikia kwake soko la pamoja la watu milioni 450 la Umoja wa Ulaya ni jambo linalofungamana na kiwango cha makubaliano yake kwa ajili ya kufuata kanuni za umoja huo.
Licha ya tahadhari zote hizo, lakini inaonekana kuwa, Uingereza imeazimia kuona uhusiano wake wa kibiashara na Umoja wa Ulaya unakuwa wa juu zaidi ya umoja huo na isijumuishwe na sheria ngumu za kibiashara, kiuchumi na ushuru wa forodha za umoja huo. Inatarajiwa kuwa, baada ya hotuba ya Boris Johnson Jumatatu iliyopita, Umoja wa Ulaya nao utatangaza matakwa yake katika hatua ya baada ya Uingereza kujiondoa katika umoja huo.

Brussels imetangaza kuwa, haina matarajio sana na jedwali za Uingereza na inaamini kuwa, makubaliano ya mwisho na London hayatakuwa na fursa kama ilivyokuwa katika kipindi ambacho nchi hiyo ilikuwa mwanachama wa umoja huo. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanadhani kwamba, hata kama Uingereza ina hamu ya kufikiwa makubaliano na umoja huo kama yale ya Australia, ni jambo lililo mbali suala hilo kufikiwa hadi mwishoni mwa mwaka huu.
Ursula von der Leyen, Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya anasema kuwa, licha ya kwamba, tuna hamu ya kuwa na uhusiano bora kabisa na Uingereza, lakini hakutakuweko uhusiano mzuri na nchi hiyo kama ilivyokuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, hatua ijayo ya mazungumzo ya Brexit itaanza mwezi ujao wa Machii.