ICC yaafiki uchunguzi kuhusu jinai za kivita za Marekani nchini Afghanistan
Oktoba mwaka 2001, kwa kisingizio cha hujuma za Sepemba 11 mwaka huo, Marekani ilianzisha uvamizi dhidi ya Afghanistan. Tokea wakati huo hadi sasa Marekani imeendelea kuikalia kwa mabavu Afghanistan na askari wake wametekeleza jinai dhidi ya raia wa nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuua raia wasio na hatia.
Hivi sasa pamoja na kuwepo mashinikizo ya pande zote ya Marekani dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), mahakama hiyo imeamua kuanzisha uchunguzi kuhusu jinai za askari wa Marekani nchini Afghanistan.
Siku ya Alhamisi Machi 2020, ICC iliamuru kuanzishwe uchunguzi kuhusu jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu nchini Afghanistan. Kwa mujibu wa hukumu hiyo ya majaji wa rufaa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi, uchunguzi utafanyika kuhusu jinai zilizotekelezwa Afghanistan kuanzia tarehe Mosi Mei 2003 nchini Afghanistan.
Uchunguzi huo utahusu uwezekano wa kuhusika wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan katika jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu. Marekani iliivamia Afghansitan kwa madai ya kukabiliana na kundi la Taliban. ICC imetoa hukumu ya kuchuguza jinai za kivita za Marekani nchini Afghanistan siku chache tu baada ya kutiwa saini mapatano baina ya Marekani na Taliban.
Mnamo Novemba 2017, Fatou Benousda mwendesha mashtaka mkuu wa ICC alitaka mahakama hiyo ianzishe uchunguzi kuhusu jinai Afghanistan baada ya uchunguzi wa awali wa miaka 10 kubaini kuhusu uwezekano wa kujiri jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu katika nchi hiyo.
Bensouda anasema: "Taarifa kuhusu askari na maafisa wa kijasusi wa Marekani nchini Afghanistan zinaoneysha wamehusika na utesaji, muamala usio na huruma, udhalilishaji wananchi, ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wafungwa wakati wa vita vya Afghansitan katika maeneo mengine katika miaka ya 2003 na 2004."
Mwaka 2018 ICC ilisajili maelefu ya malalamiko ya waathirika wa vita nchini Afghanistan na kwa msingi huo mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo amekuwa akifanya uchunguzi kuhusu jinai hizo. Suala hilo limewakasirisha sana wakuu wa Marekani ambao walibatilisha visa ya Fatou Bensouda ya kuingia Marekani.
Aprili mwaka 2019, majaji wa ICC walikiri kuwa kulifanyika jinai kubwa nchini Afghanistan lakini wakapinga uanziswaji uchunguzi kuhusu jinai hizo. Hata hivyo walikataa kuruhusu uchunguzi wa uhalifu kama huo katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita kwa madai kuwa Marekani na wahusika wengine hawangetoa ushirikiano uliotakiwa.
Uamuzi huo wa ICC ambao wakati huo ulipongezwa na Marekani ulitokana na mashinikizo ya pande zote ya wakuu wa Washington dhidi ya mahakama hiyo ya kimataifa.
Hata hivyo uamuzi huo wa ICC ulikosolewa vikali na taasisi za kimataifa za kutetekea haki za binadami ikiwamo Amnesty International. Watetezi wa haki za binadamu walisema mahakama hiyo hailipi umuhimu suala la kutendewa haki waathiriwa wa jinai za kivita wa Afghanistan.
Mwendesha mashtaka Fatou Bensouda alikata rufaa dhidi ya uamuzi wa majaji hao mnamo mwezi Septemba. Katika uamuzi wao Alhamisi, majaji wa rufaa katika ICC walisema majaji wenzao katika mahakama ya chini walifasiri vibaya kanuni za ICC wakati walipokataa Marekani ishtakiwe na kwa msingi huo wamesema uchunguzi unapaswa kuendelea.
Biraj Patnaik, mkuu wa Amnesty International katika eneo la Asia Magharibi anasema, uchunguzi kuhusu jinai za kivita nchini Afghanistan ni jukumu la kisheria na kimaadili la ICC.
Marekani imekuwa ikipinga hatua yoyote ya ICC kuchunguza jinai za askari wake nchini Afghanistan na hata imeenda mbele zaidi na kutoa vitisho dhidi ya mhakama hiyo. Suala hili linaoneysha kuwa utawala wa Trump unafahamu fika kuwa askari wake wametenda jinai za kivita na dhidi ya binadamu nchini Afghanistan.
Katika kipindi cha miaka 18 iliyopita, wanajeshi wa Marekani wametenda jinai nyingi nchini Afghanistan na hivyo wanapaswa kufikishwa kuzimbani. Kati ya mifano ya jinai za Marekani nchini Afghanistan ni kuwaua raia 17 Waafghani katika eneo la Panjwayi mkoani Kandahar tarehe 11 Machi 2012 ambapo waliteketeza moto miili ya raia hao. Pia tunaweza kuashiria hujuma ya ndege za kivita za Marekani dhidi ya hospitali ya Madaktari Wasio na Mipaka, MSF, katika mji wa Kandahar mwaka 2015 na utesaji wa wafungwa katika Jela ya Bagram na jela zingina za Marekani. Jinai hizo za Marekani zimekuwa zikikosolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Marekani ambayo inajiona kuwa kiranja wa dunia inaamini kuwa wanajeshi wake wanaotenda jinai hawapasi kufunguliwa mashtaka katika mahakama yoyote ya kimataifa.