Mar 16, 2020 02:34 UTC
  • Kushtadi mizozo kati ya Uturuki na Ugiriki

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imemwita balozi wa Ugiriki mjini Ankara na kumkabidhi malalamiko yake kufuatia ukiukaji wa haki ya kujitawala kwenye maji ya eneo hili na kadhalika kitendo cha serikali ya Athens cha kuweka vikosi vyake katika mipaka ya nchi mbili.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imemtaka Michael-Christos Diamessis, balozi wa Ugiriki mjini Ankara kuhakikisha nchi yake inakomesha ukiukaji wa haki yake ya kujitawala katika maji ya eneo ya bahari ya Mediterrania. Kwa kuzingatia uhusiano wa uhasama uliopo kati ya Ugiriki na Uturuki katika miongo kadhaa iliyopita, ni suala lililo wazi kwamba hatua ya kuitwa balozi wa Ugiriki mjini Ankara huwenda ikakabiliwa na hatua mkabala kutoka kwa Ugiriki na hivyo kuibua mzozo mpya katika uhusiano wa nchi hizo. Tofauti kati ya nchi mbili ni zenye historia ndefu, ambapo licha ya juhudi kadhaa kufanyika kwa lengo la kuboresha uhusiano huo katika duru tofauti na pia juhudi za kimataifa kwa ajili ya kutatuliwa mzozo huo, lakini bado mgogoro baina yao umeendelea kushuhudiwa. Tukiangalia uhusiano wa nchi mbili tunaweza kusema kuwa, uhusiano wa Ankara na Athens katika miongo kadhaa iliyopita hususan baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ulikuwa uliogubikwa na matatizo na tofauti kadhaa zisizotatulika.

Ugomvi kati ya watawala wa Ugiriki na Uturuki

Ukweli ni kwamba wakati fulani, uingiliaji wa ndani na uvamizi wa kijeshi na wakati mwingine, uungaji mkono kwa wapinzani wa serikali za nchi mbili, ni mambo yaliyoandaa tofauti kati ya mataifa hayo jirani. Aidha wakati fulani pia, suala la kunufaika na vyanzo vya nishati katika Bahari ya Mediterrania, na hatua ya kuwaalika wawekezaji wa kimataifa, ni mambo yaliyochochea uhasama kati yao. Pamoja na hayo, katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja uliopita, uhusiano wa nchi mbili uliingia katika hatua mpya ya mizozo mingi. Licha ya kwamba Uturuki na Ugiriki ni wanachama wenye ushawishi ndani ya Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO), lakini mizozo kati ya nchi mbili hizo jirani hususan katika mazingira ya sasa imeshtadi kiasi kwamba inatajwa kuwa hata upatanishi wa nchi nyingine mwanachama wa NATO bado haujaweza kuwa na taathira ya kupunguza tofauti zilizopo kati ya Ankara na Athens katika uwanja huo. Wakati huo huo, mizozo kati ya majirani wawili imekuwa mibaya kuhusu bahari ya Mediterrania kiasi kwamba baadhi ya weledi wa mambo wanaelezea uwezekano wa kutokea mapigano ya kijeshi kati ya pande mbili.

Licha ya kufanyika juhudi nyingi za upatanishi, lakini hazijawa na mafanikio ya kumaliza mzozo

Katika uwanja huo Angelos Sirigos mtaalamu na mchambuzi wa chama cha Kidemokrasia nchini Ugiriki anasema: "Sisi hatuwezi kuvumilia ukiukaji huu wa Uturuki kwa haki yetu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana jeshi la baharini la Ugiriki siku zote limejiweka katika hali ya maandalizi." Mkabala wale Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki pia ameitaja mienendo hiyo ya serikali ya Ugiriki kuwa ni sawa na kashfa kwa kusema: "Sababu ya mizozo hiyo, inatokana na tofauti kuhusu namna gani ya kustafidi na vyanzo vya gesi na mafuta katika upande wa mashariki mwa bahari ya Mediterrania." Kufuatia malalamiko ya Ugiriki, kisiwa cha Cyprus na baadhi ya madola ya Magharibi kutokana na operesheni za uchimbaji, uvunaji na kustafidi na vyanzo vya nishati vya upande wa mashariki mwa bahari ya Mediterrania, serikali ya Ankara sambamba na kutiliana saini na serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya makubaliano ya ushirikiano wa pande mbili katika bahari na kuchimba mafuta na gesi, ilifanya juhudi pia kuvuruga mlingano wa nguvu katika eneo. Kiujumla ni kwamba hatua ya kuitwa balozi wa Ugiriki mjini Ankara na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ni lazima itachochea tofauti za ankara na Athens katika uwanja wa mzozo wa ardhi na pia tofauti katika uwanja wa kunufaika na vyanzo vya nishati katika bahari ya Mediterrania. Suala ambalo kwa kuzingatia hisia kali za viongozi wa nchi mbili, huwenda likawa na hasara zaidi katika mwenendo wa kuboresha uhusiano kati ya Ugiriki na Uturuki.

Tags