Nancy Pelosi apinga kuahirishwa uchaguzi ujao wa rais nchini Marekani
Nancy Pelosi, Spika wa Bunge la Wawakilishi nchini Marekani, amepinga suala la kuahirishwa uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huuu.
Pelosi ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya MSNBC juu ya uwezekano wa kurejea tena virusi vya Corona na kufutwa uchaguzi wa rais, ambapo amebainisha kuwa, licha ya kuwepo hatari ya kuenea virusi vya Corona na wasi wasi walionao wananchi, lakini uchaguzi ni lazima ufanyike. Spika huyo wa Bunge la Wawakilishi la Marekani amesisitiza kuwa, Wademocrat ni lazima wafanye juhudi kuhakikisha Donald Trump hafuti uchaguzi wa mwezi Novemba. Kadhalika Nancy Pelosi ameonyesha matumaini kwamba baadhi ya wanachama wa Republican pia watapinga hatua tarajiwa ya Trump kuahirisha uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Akienedelea, amemkosoa Rais Donald Trump na kusema kuwa, amefanya mambo mengi yanayoidhoofisha Marekani na kusisitiza kuwa hatoruhusu kudhoofishwa demokrasia ya nchi hiyo. Kabla ya hapo pia kanali ya televisheni ya CNN iliripoti kwamba, akthari ya wanachama wa Democrat wana wasi wasi wa njama za Trump za kuchelewesha uchaguzi wa rais au hata kukataa kutoka ikulu ya White House hata baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Novemba.