Ongezeko la asilimia 14 la ukosefu wa ajira nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i60590-ongezeko_la_asilimia_14_la_ukosefu_wa_ajira_nchini_marekani
Ofisi ya Bajeti ya Congress ya Marekani imetoa ripoti ikionyesha kuongezeka kwa asilimia 14 ukosefu wa kazi nchini humo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 25, 2020 03:13 UTC
  • Ongezeko la asilimia 14 la ukosefu wa ajira nchini Marekani

Ofisi ya Bajeti ya Congress ya Marekani imetoa ripoti ikionyesha kuongezeka kwa asilimia 14 ukosefu wa kazi nchini humo.

Ofisi hiyo imesema kwamba ongezeko hilo la uhaba wa ajira limeripotiwa katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu wa 2020.

Hii ni katika hali ambayo mamilioni ya Wamarekani wamepoteza ajira  au wanakadiriwa kupoteza nafasi hizo za kazi katika miezi michache ijayo.

Alhamisi iliyopita, Wizara ya Kazi ya Marekani ilitoa ripoti yake ya kila wiki ikisema kuwa tayari watu milioni 26 wamepoteza nafasi zao za kazi katika kipindi cha wiki tano zilizopita kutokana na kuenea kwa kasi nchini humo virusi hatari vya corona.

Trump aliyeshindwa kupambana na maradhi corona

Kuenea virusi hivyo katika pembe zote za nchi hiyo kumepelekea viwanda na vituo vingine vya uzalishaji ajira kufungwa na hivyo kuifanya nchi hiyo ikabiliwe na mgogoro mkubwa wa kiuchumi.

Bado serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani inaendelea kukosolewa vikali kutokana na kuzembea kwake katika kukabiliana na virusi hivyo.

Marekani ndiyo inayoongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya waathirika na wahanga wa virusi vya corona.

Idadi ya watu walioathirika na vurusi hivyo nchini humo sasa imefikia watu 925,758 ambapo 52,217 kati ya yao, tayari wamekwishafariki dunia.

Wakati huo huo mgombea wa kiti cha rais wa nchi hiyo kwa tiketi ya chama cha Democrat amemkosoa vikali Trump kwa matamshi yake ya kukejeli usalama na afya ya Wamarekani.

Joe Biden, mgombea wa urais wa Marekani wa chama cha Democrat katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu, amemkosoa vikali Trump kupitia ujumbe wa mtandao wa kijamii wa Twitter, aliyewataka Wamarekani wanywe mada za kuulia vijidudumaradhi kwa ajili ya kupambana na corona.

Biden amemkosoa vikali Trump kwa matamshi yake hayo ya kejeli katika hali ambayo ripoti za kutisha zinaendelea kutolewa kuhusu idadi kubwa ya Wamarekani wanaoendelea kupoteza maisha kutokana na virusi vya corona.

Matamshi hayo yanatolewa huku wakosoaji wa Trump wakisema kwamba virusi hivyo vimeenea kwa kasi na kutoa roho za Wamarekani wengi kutokana na uzembe alioufanya Trump katika kukabilian na virusi hivyo.