Biden ambwaga Trump katika utafiti mpya wa maoni Marekani
Joe Biden, mgombea wa chama cha Democrat katika uchaguzi wa rais nchini Marekani amembwaga Rais Donald Trump katika uchunguzi mpya wa maoni uliofanyika nchini humo.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi huo uliofanywa na gazeti la USA Today kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Suffolk, Biden amepata asilimia 44 na kumshinda Trump ambaye ameambulia asilimia 38.
Biden amemshinda Trump kwa alama sita katika hali ambayo, makamu huyo wa rais wa zamani wa Marekani alimbwaga Trump kwa alama tatu katika utafiti mwingine wa maoni uliofanyika Disemba mwaka jana.
Kwa mujibu wa utafiti mpya wa gazeti la USA Today kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Suffolk, asilimia 57 ya Wamarekani wamesema kuwa Biden anawajali watu wa kawaida kama wao, ikilinganaishwa na asilimia 39 aliyoipata Trump.
Uchunguzi mwingine wa maoni uliofanywa hivi karibuni na televisheni ya CNN ulionesha kuwa umaarufu wa Trump umepungua katika wiki za hivi karibuni kutokana na uzembe wa serikali yake wa kushindwa kuzuia maambukizi ya corona na kutojiandaa vizuri kuzuia vifo vya watu.
Hivi karibuni, wananchi wa Marekani walifanya maandamano na kukusanyika mbele ya majengo ya Trump kulalamikia uzembe mkubwa aliofanya katika kukabiliana na janga la corona.
Uchaguzi wa rais nchini Marekani utafanyika mwezi Novemba mwaka huu ambapo inatazamiwa kuwa Trump wa chama tawalacha Republican atachuana na hasimu wake mkubwa wa kisiasa, Joe Biden wa Democratic.