Marekani yaondoa nchini Saudia mifumo yake ya makombora ya Patriot
https://parstoday.ir/sw/news/world-i60848-marekani_yaondoa_nchini_saudia_mifumo_yake_ya_makombora_ya_patriot
Marekani imeanza kuondoa katika ardhi ya Saudi Arabia mifumo yake ya makombora ya Patriot na zana zingine za kijeshi, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kupunguza uungaji mkono wake wa kijeshi kwa utawala huo wa kifalme.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2020 03:47 UTC
  • Marekani yaondoa nchini Saudia mifumo yake ya makombora ya Patriot

Marekani imeanza kuondoa katika ardhi ya Saudi Arabia mifumo yake ya makombora ya Patriot na zana zingine za kijeshi, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kupunguza uungaji mkono wake wa kijeshi kwa utawala huo wa kifalme.

Katika ripoti ya jana Alkhamisi, jarida la The Wall Street Journal lilinukuu maafisa wa serikali ya Washington ambao hawakutaka kutaja majina yao waliosema kuwa, mifumo minne ya makombora ya ardhini hadi angani ya Patriot, zana nyinginezo za kijeshi pamoja na maafisa wa kijeshi wa Marekani wataondolewa kutoka kwenye vituo vya mafuta vya Saudia.

Kadhalika maafisa hao wamesema Marekani inatazamiwa kupunguza vikosi vyake vya baharini katika Ghuba ya Uajemi karibuni hivi, na kwamba tayari ndege mbili za kivita za US zimeshaondolewa katika eneo hili.

Marekani ilishadidisha uwepo wa kijeshi katika eneo la Asia Magharibi mwaka jana, katika anga ya taharuki na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sehemu ya suhula na zana hizo za kijeshi za Marekani zilipelekwa Saudia mwezi Septemba mwaka jana, baada ya kujiri wimbi la mashambulizi ya makombora dhidi ya vituo vya mafuta vya Riyadh.

Taasisi za mafuta za Aramco ya Saudia zilishambuliwa kwa makombora na Ansarullah ya Yemen

Mapema mwezi uliopita wa Aprili, Rais Donald Trump alitishia kwamba, Washington itasitisha uungaji mkono wake wa kijeshi kwa Saudia, iwapo utawala huo wa kifalme hautasitisha mvutano baina yake na Russia juu ya bei ya mafuta.

Trump alitoa vitisho hivyo katika mazungumzo ya simu na Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, ambapo alisema kuwa Marekani haitakuwa na budi ila kuanza kuondoa vikosi vyake Saudia iwapo utawala wa Riyadh hautapunguza kiwango cha mafuta unachozalisha.