ICC: Vikwazo vya Marekani ni ukiukaji wa mkondo wa utekelezaji sheria
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imepinga vikwazo ilivyowekewa na Marekani na kuvitaja kuwa ni juhudi zisizokubalika katika utekelezaji sheria.
Mahakama hiyo iliyo na makao makuu yake mjini Hague Uholanzi imetoa taarifa leo Ijumaa alfajiri ikisema kuwa vikwazo hivyo ni juhudi za hivi karibuni zaidi na zisizokuwa na mfano wake zinazofanywa na Marekani dhidi ya mahakama hiyo ya kimataifa.
Tarifa hiyo inasema kuwa O-Gon Kwon, Mkuu wa Mahakama ya ICC amepinga vikali vikwazo hivyo vya Marekani na kusisitiza kuwa vinadhoofisha juhudi za mahakama hiyo za kupambana na uvunjivu wa sheria na kukwepa uwajibikaji kuhusu jinai nyingi zinazotekelezwa duniani.
Jana Alkhamisi Rais Donald Trump wa Marekani alisaini dikrii inayoruhusu maafisa wa ICC kuwekewa vikwazo. Dikrii hiyo inampa waziri wa mambo ya nje wa Marekani idhini ya kushirikiana na waziri wa fedha wa nchi hiyo katika kuzuia mali za maafisa wa ICC ambao wanahusika katika kuchunguza jinai za kivita zilizotendwa na askari wa Marekani wanaohudumu nchini Afghanistan.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia akitoa maoni yake kuhusiaa na kitendo hicho cha ubabe cha Marekani katika kuiwekea vikwazo ICC alisema jana usiku kwamba hivi sasa ICC imerubuniwa na wahalifu na wakwepaji sheria ambao wanajifanya kuwa ni wanadiplomasia.
Muhammad Zarif amekosa uamuzi huo mbovu wa Marekani na pia kimya cha jamii ya Kimaaifa mbele ya ubabe huo wa Washington.