Maandamano ya kulaani kudhalilishwa Mtume Mtukufu (saw) yafanyika Kashmir
Makumi ya wakazi wa eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan wamefanya maandamano ya kulaani kitendo cha jarida linalochapishwa nchini Ufaransa la Charlie Hebdo cha kuchapisha tena vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW).
Waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara za kulilaani jarida hilo la Kifaransa kwa kuyavunjia heshima Matukufu ya Kiislamu kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza.
Kadhalika wakazi hao wa eneo la Kashmir ambao aghalabu yao ni Waislamu wamechoma moto bendera za Ufaransa katika maandamano hayo. Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao yalikuwa na ujumbe unaosema "Koma Charlie Hebdo".
Maandamano haya yamejiri siku moja baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan kusema katika taarifa kuwa: "Tunalaani kwa nguvu zote uamuzi wa jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo wa kuchapisha tena kibonzo kinachomtusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW). Kitendo hicho cha kichochezi na kinachogusa nyoyo na hisia za mabilioni ya Waislamu kote duniani hakipaswi kuhalalishwa kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza."
Siku ya Jumatano, Chuo Kikuu cha Al Azhar nchini Misri kilitoa taarifa ya kulaani chokochoko hizo na kueleza bayana kuwa, vitendo vya namna hiyo vinarejesha nyuma jitihada za kimataifa za kuhakikisha kuwa jamii ya wanadamu inaishi kwa utangamano, maridhiano, amani na maelewano bila kujali tofauti zao za kidini.
Kwa mara nyingine tena jarida hilo la Kifaransa la Charlie Hebdo limeamua kwa makusudi kuwafanyia kejeli na istihzai Waislamu na dini tukufu ya Uislamu kwa kuchapisha vibonzo hivyo Jumatano ya juzi, siku ya kuanza kwa kesi dhidi ya watuhumiwa wa shambulizi dhidi ya ofisi ya jarida hilo mnamo Januari 7 mwaka 2015.