Amnesty: 75% ya mikutano ya kampeni za uchaguzi Marekani imeshuhudia fujo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64206-amnesty_75_ya_mikutano_ya_kampeni_za_uchaguzi_marekani_imeshuhudia_fujo
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeeleza juu ya wasi wasi mkubwa lilionao kutokana na kushtadi vitendo vya ghasia, machafuko na mapigano katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu nchini Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 24, 2020 04:22 UTC
  • Amnesty: 75% ya mikutano ya kampeni za uchaguzi Marekani imeshuhudia fujo

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeeleza juu ya wasi wasi mkubwa lilionao kutokana na kushtadi vitendo vya ghasia, machafuko na mapigano katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu nchini Marekani.

Taarifa ya Amnesty International imesema, kati ya mwezi Mei na Septemba mwaka huu, asilimia 75 ya mikutano ya kampeni za uchaguzi huko nchini Marekani imeshuhudia machafuko na mapigano baina ya makundi hasimu ya kisiasa.

Shirika hilo la Msahama Duniani limesema kinachochochea machafuko hayo katika mikusanyiko hiyo ya kisiasa nchini Marekani ni uwepo wa raia waliojizatiti kwa silaha; na kwamba waandamanaji na wapiga kura nchini humo hawana dhamana ya usalama wao.

Haya yanaripotiwa huku zikiwa zimesalia chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi wa rais wa Marekani kufanyika tarehe 3 ya mwezi ujao wa Novemba. Wadadisi wa mambo wameonya kuwa, yumkini Marekani itashuhudia machafuko makubwa ya baada ya uchaguzi.

Polisi ya US ikikabiliana na wafanya fujo katika mkutano wa kampeni mjini Boston

Wiki iliyopita, maafisa wa jimbo la Massachusetts nchini Marekani walitangaza habari ya kutokea mapigano kati ya waungaji mkono na wapinzani wa Rais Donald Trump katika mji wa Boston jimboni hapo.

Trump amekuwa akiunga mkono kila mara vitendo vya fujo na utumiaji nguvu vinavyofanywa na wafuasi na waungaji mkono wake wakuu, ambayo ni makundi ya wazungu wanaojiona bora kuliko watu wa asili nyingine, kwa ajili ya kushambulia maandamano ya wananchi wanaompinga.