Wasiwasi wa kuibuka ghasia huku siku ya uchaguzi ikikaribia Marekani
Kuna wasiwasi mkubwa kuwa kutaibuka machafuko na ghasia nchini Marekani baada ya upigaji kura siku ya Jumanne.
Olivia Katbi Smith, mkurugenzi mwenza wa Taasisi ya Democratic Socialists amenukuliwa na gazeti la Washington Post akisema, mrengo wa kulia wa Warepublican hauko tayari kuachia ngazi na hivyo kuna uwezekano wa kuibuka ghasia. Amesema watu wenye misimamo mikali katika kambi mbili hasimu za kisiasa wanaweza kukabiliana mjini Portland jimboni Oregon, mji ambao umekuwa medani ya ghasia na nembo ya mgawanyiko wa kisiasa Marekani.
Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akihimiza chuki katika mikutano yake ya kisiasa huku ununuzi wa bunduki ukivunja rekodi nchini humo.
Hivi sasa katika mitandao ya kijamii ya Marekani kuna tetesi kuwa yamkini vita vya wenywe kwa wenyewe vikaibuka nchini humo iwapo ghasia zitaibuka na kuchukua mkondo tafauti baada ya uchaguzi wa Novemba tatu.
Katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa makabiliano baina ya wanagambo wa mrengo wa kulia na wanaharakati wa kijamii kote Marekani hasa wakati wa maandamano ya kupinga ukatili wa polisi na ubaguzi wa rangi.
Huku uchaguzi nchini humo utakaofanyika Jumanne ukikaribia, uchunguzi wa maoni uliochapishwa na Washington Post unaonyesha kuwa mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha Democrat, Joe Biden anaongoza kitaifa kwa zaidi ya pointi tisa.