Nov 12, 2020 08:02 UTC
  • Iran: Ripoti mpya ya IAEA inaonyesha wakala huo unaendelea na ukaguzi nchini

Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Taasisi za Kimataifa zenye makao yao mjini Vienna Austria amesema ripoti mpya iliyotolewa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) inaonyesha kuwa taasisi hiyo ya kimataifa inaendelea kukagua na kufanyia uhakiki miradi ya nyuklia ya Iran bila vizingiti vyovyote.

Kazem Gharib Abadi amesema mbali na Jamhuri ya Kiislamu kuendelea kuzalisha na kuhifadhi maji mazito, lakini pia imeuza nje ya nchi tani 2.2 za maji hayo, huku ikitumia tani 1.3 za bidhaa hiyo katika utafiti na shughuli zake za ustawi.

Ameeleza bayana kuwa, kama ilivyoashiria ripoti hiyo ya IAEA, Iran inaendelea kurutubisha madini ya urani katika vituo vya nyuklia vya Natanz na Fordow, kwa kiwango cha asilimia 4.5, ambacho ni zaidi ya asilimia 3.67 kilichoanishwa na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Ikumbukwe kuwa, Iran ilipunguza uwajibikaji katika JCPOA, kama jibu kwa hatua ya Marekani ya kujiondoa kwenye mapatano hayo.

Gharib Abadi amesema licha ya Iran na IAEA kutofautiana katika masuala kadhaa ya kiufundi, lakini wakala huo wa Umoja wa Mataifa unaendelea na shughuli zake za ukaguzi hapa nchini, huku mashauriano ya kupatia ufumbuzi tofauti hizo za pande mbili yakiendelea.

Wakati huo huo, Majid Takht-Ravanchi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema IAEA inapaswa kutekeleza jukumu lake la ukaguzi, pasina kukiuka haki za msingi za nchi wanachama.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi alipoitembelea Iran karibuni

Ameuambia mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba, iwapo miradi ya nyuklia ya Saudi Arabia ina malengo ya amani kama inavyodai, basi serikali ya Riyadh iruhusu ukaguzi wa IAEA. Balozi huyo wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, Tehran ndiyo inayoendesha kwa uwazi zaidi shughuli zake za nyuklia zenye malengo ya amani kuliko nchi zote wanachama wa wakala huo. 

Hivi karibuni, Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) alikiri kuwa, kinyume na inavyodaiwa na Marekani, mpango wa nyuklia wa Iran unafuatilia malengo ya amani.

Tags