Wito wa kuhitimishwa sarakasi za uchaguzi wa rais wa Marekani
(last modified Sat, 14 Nov 2020 06:46:06 GMT )
Nov 14, 2020 06:46 UTC
  • Wito wa kuhitimishwa sarakasi za uchaguzi wa rais wa Marekani

Kuendelea kwa mzozo wa matokeo ya uchaguzi wa rais wa Marekani uliozushwa na Rais Donalld Trump ambaye alikuwa mgombea wa chama cha Republican katika uchaguzi huo, kupanuka mzozo huo na kutolewa madai mapya kumetajwa kuwa ni tahadhari kubwa kuhusiana na matokeo mabaya kwa Marakeni.

Spika wa Kongresi ya Marekani, Nancy Pelosi amekosoa vikali msimamo wa Warepublican wa kuchelewa kukubali kushindwa na kumtambua Joe Biden kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais na vilevile kukataa kupasisha kifurushi kipya cha kusaidia mapambano dhidi ya virusi vya corona. Pelosi ambaye Alkhamisi iliyopita alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Kongresi ya Marekani, alieleza kusikitishwa na jinsi Warepublican walivyoamua kutoheshimu maamuzi ya wananchi wa Marekani na kuwaambia: "Hitimisheni sarakati hii na anzeni kufanya kazi muhimu kwa ajili ya wananchi wa Marekani."

Pelosi alikuwa akiashiria msimamo wa baadhi ya maafisa wa ngazi za juu wa chama cha Republican akiwemo Mitch McConnell, kiongozi wa waliowengi katika Baraza la Seneti. Jumanne iliyopita McConnell baada ya kuchaguiwa tena kuwa kiongozi wa waliowengi katika seneti ya Marekani aliunga mkono madai ya Donald Trump ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo. 

Nancy Pelosi

Katika ujumbe wake wa Twitter Alkhamisi iliyopita Trump alikariri madai ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi wa rais na kusema, mfumo wa kupigia kura wa Marekani umefuta kura zake milioni 2.7. Trump hayuko peke yake katika kuzusha mzozo huo wa uchaguzi wa rais nchini Marekani bali anaungwa mkono na baadhi ya maafisa wakubwa wa Republican.

Kuendelea mgogoro huo wa kisiasa kumeporomosha zaidi nafasi na hadhi ya kisiasa ya Marekani ambayo katika kipindi cha utawala wa Donald Trump imeshuka chini kwa kiwango kikubwa kutokana na mienendo na siasa za kiongozi huyo. Kwa sasa nchi nyingi zinajiuliza kwamba, Marekani ambayo daima imekuwa ikijitangaza kuwa kinara wa demokrasia na uhuru, imepatwa na nini kiasi kwamba rais wake anatangaza waziwazi kuwa, mfumo wa uchaguzi wa nchi hiyo ni wa kifisadi na kwamba kumefanyika wizi na udanganyifu katika zoezi la uchaguzi wa rais, na hatimaye anahoji na kushuku mfumo mzima wa uchaguzi wa Marekani? Hapana shaka yoyote kwamba, suala hilo ni ishara ya kuanza kusambaratika dola la Marekani kisiasa na kimaadili. 

Hii ni pamoja na kuwa, mzozo huo ulioanzishwa na Trump umewafanya Wamarekani wapoteze imani yao kwa mfumo wa uchaguzi wa nchi hiyo. Hii ni kwa sababu, kutokana na mgawanyiko uliojitokeza katika jamii ya Marekani kuhusu usahihi wa uchaguzi wa rais, sheria zake na utendaji wa maafisa wa uchaguzi, sasa wananchi wamepoteza imani yao kwa mfumo wa uchaguzi wa nchi hiyo. Jambo linalotia wasiwasi zaidi ni kuwa, zaidi ya nusu ya Wamarekani wanatazamia kuwa, iwapo Joe Biden atakuwa rais wa nchi hiyo, mchakato wa kukabidhiana madaraka baina yake na Donald Trump hautafanyika kwa amani.

Biden na Trump

Wavuti ya The Hill ya Kongresi ya Marekani imeashiria hatua zinazoweza kuchukuliwa na Donald Trump kama rais anayeondoka ikiwa ni pamoja na kukataa kuondoka ikulu ya White House, kuanzisha mgogoro wa kisiasa wa kimataifa, kuitumbukiza Marekani katika machafuko ya kisiasa na hatimaye kuibua matatizo katika mchakato wa kukabidhi madaraka kwa Joe Biden.

Katika upande mwingine hali ya mkanganyiko ya sasa na mienendo isiyo ya kawaida ya Trump ya kukataa kuanza mchakato wa kukabidhi madaraka ya nchi kwa Biden na hata kukataa kumpatia mrithi wake taarifa za kila siku kama rais mteule, vimekosolewa pia na hata baadhi ya maafisa wa chama cha Republican. 

Nchi mbalimbali za dunia pia zimechanganyikiwa kuhusiana na nani rais ajaye wa Marekani. Kwa mfano tu, wakati nchi nyingi za Ulaya na China zimempongeza Biden kwa kushinda uchaguzi wa rais wa Marekani, Russia imetangaza kuwa, itasubiri kukamilishwa zoezi la kuhesabiwa kura na tangazo la mwisho la matokeo ya uchaguzi huo. 

Hali hii imepiga kengele ya hatari ndani ya Marekani. Kundi la maafisa 161 wa zamani wa usalama wa taifa akiwemo aliyewahi kuwa waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel, mkurugenzi wa zamani wa shirika la ujasusi la CIA na Wakala wa Usalama wa Taifa Jenerali Michael Hayden, jenerali mstaafu Wesley K. Clark na balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power wameandika barua wakitahadharisha kuwa, "kuchelewa serikali ya Trump kumtambua rasmi Joe Biden kama rais mteule ni hatari kubwa kwa usalama wa taifa wa Marekani."

Donald Trump

Licha ya hayo yote Trump amekataa kukubali matokeo ya uchaguzi wa rais na anawachochea waungaji mkono wake kufanya maandamano mitaani wakipinga matokeo ya zoezi hilo na kufungua mashtaka mahakamani kwa madai ya kufanyika udanganyifu.