Marekani yaweka rekodi mpya ya vifo vya Covid-19
Marekani imeweka rekodi mpya ya kutisha ya vifo na maamukizi ya ugonjwa wa Covid-19, ambapo watu 3,700 wameaga dunia kwa maradhi hayo ya kuambukiza, huku kesi mpya 250,000 zikisajiliwa ndani ya masaa 24 jana Jumatano.
Kwa mujibu wa takwimu za Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, idadi hiyo mpya ya vifo imepelekea idadi jumla ya wahanga wa virusi vya corona nchini humo kufikia 314,500.
Inakadiriwa kuwa, karibu asilimia tano ya Wamarekani, sawa na watu milioni 17 wameambukizwa ugonjwa wa Covid-19, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kurekodiwa na nchi yoyote ile duniani. Marekani ingali inaongoza kwa idadi ya vifo na maambukizo ya corona duniani.
Utendaji dhaifu wa Rais Donald Trump wa Marekani katika kushughulikia janga la corona nchini humo umekosolewa pakubwa ndani ya nchi hiyo.
Wakati huo huo, idadi ya watu wanaombukizwa virusi hatari vya corona inazidi kuwa kubwa barani Ulaya wakati huu nchi za bara hilo zikikaribia kuingia kwenye msimu wa baridi kali.
Hivi karibuni Ulaya ilikumbwa na wimbi la pili la maambukizo ya corona na nchi nyingi za bara hilo zinakabiliwa na changamoto kubwa za kukabiliana na ugonjwa huo.