Mwakilishi wa Texas: Kutatokea mzozo mkubwa katika Seneti iwapo Warepublican watashindwa
-
Chip Roy
Mwakilishi wa chama cha Republican katika Kongresi ya Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican ametahadharisha kuwa kutatokea mzozo mkubwa iwapo Warepublican wenzake watashindwa kupata wingi wa viti vya Baraza la Seneti.
Chip Roy ameambia televisheni ya Fox News kwamba, iwapo Wademokrati wataibuka na ushindi katika duru ya pili ya uchaguzi wa Baraza la Seneti katika jimbo la Georgia, basi kutaibuka mzozo mkubwa sana.
Matamshi ya mwakilishi huyu wa Kongresi ya Marekani yametolewa huku kukitarajiwa mchuano mkubwa katika uchaguzi wa duru ya pili wa Baraza la Seneti unaofanyika leo katika jimbo Georgia.
Rais Donald Trump wa Marekani jana Jumatatu alishiriki katika kampeni za uchaguzi wa seneti katika jimbo hilo katika jitihada za kuhakikisha chama tawala cha Republican kinaibuka na ushindi. Iwapo Wademocrati watashinda viti viwili vya jimbo hilo watawapokonya Warepublican udhibiti wa Barazala la Seneti.
Kwa sasa Warepublican wana viti 50 vya seneti huku wapinzani wao wa chama cha Democratic wakiwa na viti 48 kati ya viti vyote mia moja vya Baraza la Seneti.