Kila sekunde 33 Mmarekani anapoteza maisha kutokana na COVID-19
Marekani imeweka rekodi mpya kwa idadi ya watu wanaofariki kutokana corona au COVID-19 kwa siku ambapo Jumanne watu 3,936 walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha John Hopkins, katika kipindi cha wiki moja iliyopita, kwa wastani watu 2,637 wamekuwa wakifariki dunia kila siku kutokana na corona nchini Marekani. Kwa msingi huo, kila sekunde 33 mtu moja amekuwa akifariki dunia nchini Marekani kutokana na corona.
Mwezi uliopita wa Disemba ulikuwa mbaya zaidi ambapo watu 77,572 walipoteza maisha nchini Marekani kutokana na corona. Idadi ya vifo imetabiriwa kuongezeka kutokana na kuongezeka kiwango cha maambukizi na watu wanaolazwa hospitalini.
Siku ya Jumatatu iliyopita, kuliripotiwa idadi kubwa zaidi ya watu kuwahi kulazwa hospitalini nchini Marekani tokea janga la corona lianze ambapo watu 128, 210 walilazwa katika hospitali mbali mbali kote Marekani.
Madaktari Marekani wameingiwa na wasiwasi kuwa kuenea kwa kasi corona kutapelekea hospitali zishindwe kukabiliana na wimbi la wagonjwa na hivyo vifo vitaongezeka.
Hayo yanajiri wakati ambao ni watu milioni 4.5 tu waliopokea dozi ya kwanza ya chanjo ya corona Marekani kati ya watu wote milioni 331 nchini humo. Aidha hadi sasa ni dosi milioni 15.4 ambazo zimesambazwa kote Marekani.
Kwingineko, Ujerumani inatarajiwa leo kurefusha muda wa hatua kali za kudhibiti maambukizi ya corona, wakati Kansela Angela Merkel akitarajiwa kufanya mkutano kwa njia ya video na mawaziri wakuu wa majimbo 16 ya nchi.
Nchini Uingereza nako, serikali imesema masharti mapya ya kupambana na virusi vya corona huenda yakaendelea kuwepo hadi mwezi Machi, baada ya waziri mkuu Boris Johnson kusema usiku wa kuamkia leo kuwa moja kati ya wakaazi 50 wa Uingereza amepatwa na maambukizi ya corona.