Machafuko kushuhudiwa katika majimbo 50 ya Marekani kabla ya kuapishwa Biden
https://parstoday.ir/sw/news/world-i65724-machafuko_kushuhudiwa_katika_majimbo_50_ya_marekani_kabla_ya_kuapishwa_biden
Jarida linalochapishwa na Shirika la upelelezi la Marekani (FBI) limetahadharisha kuwa, magenge ya uhalifu yaliyojizatiti kwa silaha yanajiandaa kuibua ghasia na machafuko katika majimbo 50 ya nchi hiyo, kuelekea siku ya kuapishwa Rais mteule wa nchi hiyo Joe Biden, Januari 20.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 12, 2021 04:29 UTC
  • Machafuko kushuhudiwa katika majimbo 50 ya Marekani kabla ya kuapishwa Biden

Jarida linalochapishwa na Shirika la upelelezi la Marekani (FBI) limetahadharisha kuwa, magenge ya uhalifu yaliyojizatiti kwa silaha yanajiandaa kuibua ghasia na machafuko katika majimbo 50 ya nchi hiyo, kuelekea siku ya kuapishwa Rais mteule wa nchi hiyo Joe Biden, Januari 20.

Kwa mujibu wa shirika la habari la ABC News, magenge hayo ya uhalifu yanayomuunga mkono Donald Trump yanatazamiwa kuzusha vurugu za kupinga mpango wa kuondolewa madarakani rais huyo kabla ya muhula wake kukamilika rasmi kwa kutumia kipengee cha 25 cha katiba ya nchi hiyo.

FBI imesema imepokea taarifa za kiitelijensia zinazoashiria kuwa, genge moja lenye misimamo mikali linalomuunga mkono Trump linatazamiwa kuelekea katika mji mkuu Washington DC Januari 16, kufanya eti 'mapinduzi' iwapo Kongresi ya nchi hiyo itatekeleza azma yake ya kumuuzulu Trump kabla ya Januari 20.

Mashinikizo ya kumtaka Trump ajiuzulu, aondolewe madarakani au auzuliwe yanazidi kuongezeka ndani ya Marekani tangu wafuasi wake walipovamia jengo la Kongresi siku ya Jumatano tarehe 6 Januari na kulihodhi kwa saa kadhaa.

Wafuasi wa Trump waliojizatiti kwa silaha

Watu wasiopungua watano akiwemo askari polisi mmoja waliuawa kutokana na mtafaruku na machafuko yaliyosababishwa na uvamizi huo na kumfanya rais mteule wa nchi hiyo Joe Biden aitaje Jumatano hiyo ya tarehe 6 Januari, 2021 kuwa ni "siku mbaya zaidi ya historia ya Marekani".

Maafisa wengi wa serikali ya Trump wakiwemo mawaziri wa usalama wa ndani, uchukuzi na elimu wamejiuzulu kulalamikia kitendo hicho cha kushambuliwa Kongresi ya nchi hiyo na wafuasi sugu wa Trump.