Ulyanov: Mafanikio ya awali yamepatikana katika kikao cha Vienna
Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao yake mjini Vienna amesema kuwa kumepatikana mafanikio ya awali katika kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA katika mji mkuu wa Austria.
Kupitia mtandao wake wa twitter, Mikhail Ulyanov ametangaza kumalizika kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA katika mji mkuu wa Austria na kueleza kuwa, pande husika katika mapatano ya JCPOA zimechunguza mashauriano yaliyofanywa na wataalamu Jumanne wiki hii na kuridhia hatua za awali zilizopigwa.

Ulyanov amebainisha kuwa, kikao kinachofuata cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA kwa ajili ya kuendeleza harakati hiyo chanya kitafanyika wiki ijayo.
Mazungumzo ya pili ya ana kwa ana ya Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA ambayo yalianza siku ya Jumanne wiki hii huko Vienna yamefanyika jana. Ajenda kuu iliyojadiliwa katika kikao hicho ilikuwa kuhusu kuwalisha ripoti za majadiliano ya kiufundi yaliyofanywa kwenye vikao vya makundi ya wataalamu na kuondoa vikwazo.
Katika kikao hicho cha leo, wawakilishi wa Umoja wa Ulaya wakiwa ni waratibu wa mazungumzo ya kitaalamu wamewasilisha kwa wananchama wa Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA ripoti ya mashauriano ya wataalamu wa Iran na wa nchi za kundi la 4+1.