Waindonesia waandamana kulaani uungaji mkono wa US kwa Israel
Wananchi wa Indonesia wamefanya maandamano nje ya ubalozi wa Marekani na ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Jakarta kulalamikia na kulaani uungaji mkono wa Marekani kwa jinai za utawala haramu wa Israel.
Maelfu wamejitokeza kwenye maandamano hayo baada ya Swala ya Ijumaa, ambapo wameandamana katika barabara kuu zinazoelekea katika majengo yenye ubalozi wa US na ofisi za UN katika mji mkuu, Jakarta.
Baadhi ya waandamanaji walikuwa wamebeba bendera za Palestina, na mabango yenye jumbe za kuonyesha uungaji mkono wao kwa wananchi madhulumu Wapalestina.
Aidha baadhi ya mabango hayo yalikuwa na jumbe za kuulaani utawala wa Kizayuni wa Israel na kitendo cha Marekani cha kuukingia kifua utawala huo unaotenda jinai za kutisha kila uchao dhidi ya Waislamu wasio na ulinzi wa Palestina.
Bango moja lilikuwa na ujumbe unaosema "Israel, gaidi halisi, Waindonesia wamesimama na Wapalestina."

Indonesia, taifa lenye idadi kubwa zaidi ya jamii ya Waislamu duniani, haina uhusiano wa kidiplomasia na utawala pandikizi wa Israel, na kwa muda mrefu, imekuwa muungaji mkono mkubwa wa Wapalestina.
Hivi karibuni, Rais Joko Widodo wa nchi hiyo alilaani vikali mashambulizi ya anga yaliyofanywa hivi karibuni na ndege za kivita za utawala haramu wa Israel, dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Wapalestina zaidi ya 250 waliuawa shahidi katika jinai hiyo mpya ya Wazayuni.