Sisitizo la Moscow la kuiunga mkono kijeshi Caracas
(last modified Fri, 25 Jun 2021 02:14:29 GMT )
Jun 25, 2021 02:14 UTC
  • Sergei Lavrov
    Sergei Lavrov

Russia siku zote imekuwa moja kati ya waungaji mkono wakubwa wa Venezuela kimataifa licha ya mashinikizo na vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi hiyo. Vilevile inaendelea kuisaidia serikali ya Caracas na kuipa misaada ya aina mbalimbali hasa katika sekta ya ustawi wa kiuchumi na kijeshi sambamba na kumuunga mkono na kumhami Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro.

Katika uwanja huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov amefanya mazungumzo na mwenzake wa Venezuela Jorge Arreaza na kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa, Russia inaiunga mkono kikamilifu serikali ya Caracas katika mgogoro wa kisiasa wenye lengo la kuipindua serikali halali ya Rais Nicolas Maduro na kwamba jeshi la Venezuela linazo  silaha kutoka Russia. Ravrov ameongeza kuwa,  wataalamu wa Russia wanafanya kazi huko Venezuela, na kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa baina ya pande mbili wanachukua hatua za lazima na zinazohitajika kutunza zana hizo.

Russia na Venezuela miaka kadhaa iliyopita pia zilisaini hati 12 za ushirikiano katika nyanja za fedha, nishati na masuala ya kijeshi na pia katika sekta ya afya, tiba na chakula.  

Katika miaka ya karibuni Marekani imezidisha mashinikizo kwa Venezuela lengo likiwa ni kumuondoa madarakani Rais Nicolas Maduro na serikali yake ya mrengo wa kulia na kisha kuisimika madarakani serikali kibaraka ili kudhamini maslahi ya Washington. Moscow imekuwa na msimamo wa kuitetea Venezuela mkabala wa Washington na imeshasema mara kadhaa kwamba, ni wananchi wa Venezuela pekee ambao wanaweza kuchukua maamuzi ya kuanisha mustakbali wa nchi yao, na kwamba uingiliaji wa nchi ajinabi nchini humo haukubaliki. Kuhusiana na suala hilo, Sergei Ryabkov Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kuwa: Kadhia ya sasa ya Venezuela inapasa kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya amani, ya kisiasa na kupitia meza ya mazungumzo. 

Sergei Ryabkov

Viongozi wa Russia pia wamewatahadharisha mara kadhaa wenzao wa Marekani kuhusu kuendeleza sera na siasa zao za kiuhasama dhidi ya Venezuela. Hata hivyo Washington ingali inaendeleza siasa zake hizo, kuweka mashinikizo ya kiuchumi na vikwazo vikali katika nyanja mbalimbali za kiuchumi dhidi ya Venezuela zikiwemo nyanja za nishati, benki na bima. Wakati huo huo hatua ya kumuunga mkono waziwazi Juan Guaidó kiongozi wa upinzani nchini Venezuela ni sehemu ya siasa hizo ambazo zimekuwa zikitekelezwa na  Washington ili kubadili uongozi huko Venezuela bila ridhaa ya wananchi. Si hayo tu bali Washington imetishia kuishambulia kijeshi Venezuela na hivi sasa inaendeleza vikwazo dhidi ya nchi hiyo katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa COVID-19 ili kuilazimisha serikali ya mrengo wa kulia ya Maduro iondoke madarakani. Mashinikizo yote hayo yamekosolewa pakubwa na Rais huyo wa Venezuela ambaye amevitaja vikwazo vya kidhalimu vya Washington dhidi ya nchi yake kuwa ni "mauaji ya kiuchumi." 

Licha ya mashinikizo hayo yote lakini hadi sasa serikali ya Maduro ambayo inaungwa mkono na wananchi, imefanikiwa kutatua baadhi ya matatizo ya kiuchuni ya nchi hiyo yaliyosababishwa na mashinikizo ya Marekani kwa kuimarisha uhusiano wake na nchi kama Russia, China na Iran. Wakati huo huo uhusiano wa Russia na Venezuela umeimarika zaidi katika sekta za kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Katika masuala ya kijeshi sasa Russia inadhamini mahitaji ya zana za kivita za Venezuela na kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa nchi hiyo. Vilevile Russia inafanya jitihada kubwa za kuhakikisha kwamba, inaimarisha zaidi uwezo wa kijeshi wa Venezuela katika eneo la America ya Latini ili iweze kukabiliana na vitisho vya kijeshi vya Marekani.

Maduro na Putin

Jarida la Military Watch limeandika kuwa: Venezuela imefanikiwa kuwa nguvu halisi ya kijeshi katika eneo la America ya Latini licha ya kuzingirwa na mashinikizo ya Marekani. Sasa Venezuela ndiyo yenye nguvu muhimu zaidi ya anga katika eneo hilo.

Inaonekana kuwa kuimarishwa uhusiano baina ya Moscow na nchi waitifaki wake kunaweza kupunguza kiwango cha mashinikizo ya kiuchumi ya Washington kwa nchi hizo na kuboresha hali yao hasa katika kipindi hiki ambapo maafisa wa serikali ya Washington wanafanya jitihada kubwa za kuendelea kuitisha na kuitia woga nchi hiyo na kushikilia mali na fedha zake.     

Tags