Madai ya Taliban ya kuwepo serikali jumuishi nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i76914-madai_ya_taliban_ya_kuwepo_serikali_jumuishi_nchini_afghanistan
Kaimu waziri wa mambo ya nje wa serikali ya muda ya Taliban amekataa wito wa jamii ya kimataifa unaosisitizia ulazima wa kuundwa serikali jumuishi nchini Afghanistan na kudai kwamba, serikali ya Taliban ni jumuishi na ndani yake wamo wawakilishi wa jamii zote za nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 15, 2021 02:46 UTC
  • Mawlawi Amir Khan Muttaqi
    Mawlawi Amir Khan Muttaqi

Kaimu waziri wa mambo ya nje wa serikali ya muda ya Taliban amekataa wito wa jamii ya kimataifa unaosisitizia ulazima wa kuundwa serikali jumuishi nchini Afghanistan na kudai kwamba, serikali ya Taliban ni jumuishi na ndani yake wamo wawakilishi wa jamii zote za nchi hiyo.

Mawlawi Amir Khan Muttaqi ameyasema hayo katika taasisi ya mitalaa ya kistratejia ya Pakistan na kuongeza kwamba, jamii ya kimataifa inafanya kila njia ili Taliban iwaingize wapinzani wake serikalini, lakini hicho ni kitu ambacho hakiwezekani.

Kaimu waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Taliban amesema, jamii ya kimataifa inalitumia suala la haki za binadamu na sisitizo la kuundwa serikali jumuishi kwa malengo yake ya kisiasa.

Mawlawi Amir Khan Muttaqi

Amir Khan Muttaqi ametoa madai ya kuwepo serikali jumuishi nchini Afghanistan katika hali ambayo madai hayo hayakubaliwi, si ndani ya nchi hiyo wala katika nchi zingine pamoja na asasi za kimataifa.

Ijapokuwa katika siku za awali na mara baada ya kushika hatamu za utawala Taliban ilitoa ahadi ya kuunda serikali jumuishi nchini Afghanistan, lakini baada ya kutangazwa orodha ya mawaziri wa serikali ya kundi hilo ilibainika kuwa mawaziri wote hao wameteuliwa kutoka jamii moja tu au ya watu wenye mtazamo maalumu wa kisiasa; na Waafghani wa jamii zingine hawazingatiwi wala kupewa nafasi yoyote ya maana katika serikali ya Afghanistan.

Baada ya kupita karibu miezi minne tangu ilipoangushwa serikali ya Muhammad Ashraf Ghani na hatamu za utawala kuingia mikononi mwa kundi la Taliban, mamlaka yote ya uongozi nchini Afghanistan kwa sasa yanadhibitiwa na kundi hilo na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa ili kuzishirikisha jamii na makundi mengine ya kisiasa na kidini katika nchi hiyo.

Wanamgambo wa Taliban

Kuhusiana na nukta hiyo, washauri na makatibu wa masuala ya usalama wa taifa wa nchi saba za kanda hii walipitisha azimio mwishoni mwa kikao chao kilichofanyika wiki iliyopita katika mji mkuu wa India, New Delhi, lililosisitiza udharura wa kuundwa serikali yenye uwazi na jumuishi na itakayoendana na matakwa ya watu wote wa Afghanistan.

Kauli ya kaimu waziri wa mambo ya nje wa Afghanistan kuhusu kuwepo serikali jumuishi na inayoshirikisha jamii za watu wote, mbali na kuwa ni jibu la kuukataa wito wa jamii ya kimataifa wa kuundwa serikali itakayojumuisha kaumu na makabila mbalimbali ya Afghanistan, ni sisitizo pia la kuendelezwa mkakati unaotekelezwa hivi sasa na Taliban wa kuhakikisha nchi hiyo inaendeshwa na watu wenye fikra na mtazamo maalumu na wa aina moja tu.

Kwa maneno mengine ni kwamba, kinyume na mtazamo wa jamii ya kimataifa ambayo inaamini kuwa serikali ya sasa ya Taliban haiakisi mitazamo na fikra za jamii tofauti za Afghanistan, viongozi waandamizi wa kundi hilo wanaitakidi kuwa serikali ya sasa ya nchi hiyo ni serikali jumuishi iliyoshirikisha watu wa jamii zote.

Mazungumzo ya Taliban na wawakilishi wa asasi za kimataifa

Kwa kutilia maanani tofauti hiyo ya mtazamo iliyopo kati ya Taliban na jamii ya kimataifa kuhusu sura ya serikali ya sasa ya Afghanistan, inavyoonekana, changamoto ya hivi sasa kuhusu kuitambua serikali ya Taliban ingali itaendelea kuwepo.

Serikali ya Taliban inajaribu kufanya juu chini ili kuishawishi jamii ya kimataifa ilikubali na kulitambua rasmi kundi hilo kuwa ndilo linaloongoza utawala mpya wa Afghanistan, lakini ukiondoa nchi chache mno, akthari ya nchi duniani haziko tayari katika mazingira ya sasa kuitambua serikali ya Taliban; na zinatakidi kuwa kuutambua utawala wa kundi hilo kutategemea kubadilisha Taliban muelekeo wake katika masuala ya uhuru wa watu binafsi na wa kijamii na vilevile kuandaa mazingira ya kuzishirikisha jamii na mirengo yote katika utawala.../