Kupitishwa na Bunge la Uingereza sheria ya kibaguzi dhidi ya wahamiaji
Bunge la Uingereza limepitisha sheria tatanishi ya "Utaifa na Mipaka", Nationality and Borders kwa kura 298 za wabunge waliounga mkono dhidi ya 231 walioupinga mswada wa sheria hiyo.
Kwa mujibu wa sheria hiyo iliyopitishwa kwenye kikao cha Jumatano tarehe 8 Desemba, waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza atakuwa na uwezo, tena bila kutangulia kutoa taarifa, wa kufuta uraia wa Waingereza wasio Wazungu. Aidha, atakuwa na mamlaka ya kuzuia wakimbizi kuingia nchini humo.
Serikali ya London inadai kuwa, sheria hiyo itaisaidia nchi hiyo kudhibiti mipaka yake na kuzuia wahajiri haramu kuingia nchini humo. Kwa mujibu wa sheria hiyo, kanuni za uhajiri zitakuwa kali zaidi, kwa watu wanaotaka kuomba hifadhi ya ukimbizi kutakiwa wafanye hivyo wakiwa nje ya nchi hiyo. Kwa wakimbizi wanaotaka kuingia Uingereza kwa kutumia mitumbwi midogo kupitia njia ya baharini ya Kanali ya Uingereza yaani English Channel, wao watakabiliwa na vikwazo na vizuizi vikali zaidi. Kulingana na sheria ya Utaifa na Mipaka, serikali ya London itakuwa na uwezo wa kuwazuia wakimbizi katikati ya bahari na kuwazuia wasiingie Uingereza.
Baada ya kutekelezwa makubliano ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit, London imeanza kuchukua hatua na kutekeleza sera za uwekaji mipaka katika masuala ya uhamiaji na kushadidisha kanuni za kupokea wakimbizi, ikitilia mkazo zaidi kuzuia kuingia nchini humo wakimbizi wanaotumia Kanali ya Uingereza, ijulikanayo pia kwa Kifaransa kama La Manche.
Ni suala hilo, na kwa kuzingatia kutokea ajali za mara kwa mara za kuzama boti na mitumbwi iliyobeba wahamiaji, ndilo lililogeuka kuwa chanzo cha mvutano kati ya Uingereza na Ufaransa. Uhusiano wa nchi mbili hizo umeharibika zaidi hasa baada ya ajali mbaya iliyotokea katika njia hiyo ya baharini ya La Manche ambayo ilisababisha vifo vya zaidi ya wahajiri 27.
Badala ya Uingereza kutafuta suluhisho la msingi la tatizo sugu la wakimbizi na wahajiri haramu wanaokimbilia nchini humo, inataka kuwabebesha wengine mzigo wa lawama kwa kuituhumu Ufaransa kuwa ndio inayowapeleka wakimbizi hao nchini humo, ili kufifisha na kuficha sababu halisi za suala hilo. Hivi sasa, na baada ya kupitishwa sheria hiyo tatanishi na inayolalamikiwa iliyo dhidi ya wahajiri, serikali ya London inajipanga kukabiliana na wahajiri hao katika Kanali ya Uingereza, jambo ambalo bila shaka yoyote litakuja kusababisha maafa mengine mapya kwa wakimbizi katika siku za usoni.
Lakini upande mwingine wa sheria hiyo tatanishi ya "Utaifa na Mipaka" ni sura yake ya ubaguzi wa rangi. Imeelezwa katika sheria hiyo kwamba, serikali ya Uingereza itakuwa na uwezo wa kubatilisha uraia wa wananchi wake wasio Wazungu. Jambo hili, si tu linathibitisha kuwepo ubaguzi kati ya raia kwa kuwagawa katika makundi mawili ya Wazungu na wasio Wazungu, lakini pia ni ukiukaji wa haki za binadamu kulingana na vipengele vilivyobainishwa kwenye Hati ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu. Kwa sababu hiyo, yamezuka malalamiko kadhaa ndani ya bunge la Uingereza wakati wa kujadiliwa mswada wa sheria hiyo.
Wakati serikali ya chama cha Wafidhina ilipowasilisha mswada wa sheria hiyo kwenye kamati ya haki za binadamu ya bunge, wajumbe wa kamati hiyo walionya kuwa mswada huo unapingana na haki za binadamu. Wakati mswada huo ulipojadiliwa bungeni, Imran Hussain, mbunge wa Bradford kwa tiketi ya chama cha Leba, ambaye yeye mwenyewe ni Muingereza mwenye asili ya Asia, alikosoa vikali sheria zinazopinga uhajiri nchini humo na akamuuliza waziri mkuu Boris Johnson, lini atachukua hatua ya kuwatimua watu kama yeye? Imran Hussain alikwenda mbali zaidi kwa kusema: kwa sheria hizi ambazo zimependekezwa na serikali, yamkini karibuni hivi uraia wa wabunge wote wasio Wazungu utabatilishwa na kufika zamu yake yeye pia akiwa ni mbunge ya kufukuzwa nchini.
Kuibuliwa suali hilo, tena na mtu ambaye ni mbunge, ni ishara ya wazi kwamba sheria hiyo ni ya kibaguzi na si ya haki na uadilifu. Sheria ya Utaifa na Mipaka inaipa mamlaka serikali, na kwa kisingizio chochote kile, ya kufuta uraia wa Waingereza wasio Wazungu hata kama watakuwa wabunge na wana kinga ya kibunge. Nukta ya kuzingatiwa zaidi ni kwamba, mbali na kauli za wabunge kadhaa wa chama tawala cha Wahafidhina waliokuwemo bungeni, wakati Boris Johnson alipokuwa akimjibu Imran Hussain suali lake alimwambia: "Kauli hii ni ya kuaibisha na inapasa uifute". Hiyo ikiwa na maana kwamba, badala ya chama tawala cha Wahafdidhina na waziri mkuu wa Uingereza kuona haya kwa kuwasilisha na kupitisha sheria ya kibaguzi, wamewataka waathirika watarajiwa wa sheria hiyo waombe radhi wao kwa kuilalamikia.../