Putin: US, EU ziwajibishwe dunia ikitumbukia kwenye baa la njaa
(last modified Sat, 18 Jun 2022 11:29:57 GMT )
Jun 18, 2022 11:29 UTC
  • Putin: US, EU ziwajibishwe dunia ikitumbukia kwenye baa la njaa

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema ukoloni mamboleo ndio umesababisha migogoro wa kibinadamu inayoshuhudiwa katika sehemu mbalimbali duniani; na kwamba Marekani na nchi za Ulaya ndizo zinazopaswa kubebeshwa dhima iwapo dunia itatumbukia kwenye baa la njaa.

Putin alisema hayo jana Ijumaa katika hotuba inayotajwa kuwa muhimu na kueleza kuwa, usimamizi mbaya wa Wamagharibi kwa uchumi wa dunia na kuyanyonya mataifa dhaifu ndiyo sababu kuu ya kushuhudiwa mfumko wa bei za bidhaa na mgogoro wa chakula duniani.

Amesema Wamagharibi ndio walioisababishia dunia matatizo ya kiuchumi yanayoshuhudiwa hivi sasa, na kuwaweka mamia ya maelfu ya watu katika hatari ya kukumbwa na utapiamlo.

Rais wa Russia amesisitiza kuwa, "ongezeko la bei ya mafuta duniani, mfumko wa bei za bidhaa, migogoro ya chakula, gesi na mafuta yote hayo yametokana na makosa ya kimfumo kwenye sera ya uchumi ya utawala wa sasa wa Marekani, na madola ya Ulaya."

Putin amesema nchi za Magharibi zimevuruga uchumi wa dunia, kwa kuchapisha kiwango kikubwa cha fedha ili kujaribu kufufua chumi zao, sambamba na kuzitumia fedha hizo kununua bidhaa kutoka nchi za kigeni.

Amesema matatizo ya kiuchumi yanayoshuhudiwa duniani hivi sasa hayajaanza leo au miezi 3 au 4 iliyopita kama yanavyodai baadhi ya madola ya kibeberu, lakini majungu ya migogoro hiyo imekuwa ikipikwa na Wamagharibi kwa miongo mingi sasa. 

Tangu ilipoanza operesheni ya kijeshi ya Russia dhidi ya Ukraine, Marekani na waitifaki wake wameshadidisha vikwazo na mashinikizo dhidi ya Moscow. Russia nayo imejibu mapigo kwa kuwawekea vikwazo viongozi na maafisa wengi wa nchi za Magharibi.