Jul 09, 2022 11:03 UTC
  • Mahujaji waendelea na ibada ya Hija, waanza amali ya kumpiga mawe shetani, Mina

Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, kuanzia asubuhi ya leo Jumamosi wameanza amali ya kumpiga mawe Shetani huko Mina, karibu na mji mtakatifu wa Makka, katika siku ya kwanza ya Idul Adha, wakiwa mbioni kuhitimisha vipengee vikuu vya ibada ya Hija ya mwaka huu.

Tangu asubuhi na mapema, vikundi vya Waislamu vimepitia katika Bonde la Mina, magharibi mwa Saudi Arabia kwa ajili ya kurusha kokoto saba kwenye mwamba unaowakilisha vishawishi vya Shetani. Baada ya kukamilika amali hiyo ya Hija, mahujaji huchinja mnyama wa dhabihu na kisha kunyoa au kupunguza nywele zao.

Baadaye, wageni hao wa Mwenyezi Mungu walitazamiwa kuelekea Makka kwa ajili ya kufanya Tawaful- Ifadha, ambayo ni moja ya nguzo za Hija, na kisha watarudi Mina ambako watalala siku tatu za Tashreeq. Katika siku hizo watapiga mawe miamba mitatu (Jamarat) inayowakilisha shetani mlaaniwa.

Eneo la Mash'ar huko Mina liko kati ya Makka na Muzdalifah, kilomita 7 kaskazini mashariki mwa Masjidul Haram, ndani ya mipaka ya Haram. Ni bonde lililozungukwa na milima upande wa kaskazini na kusini, na haliwi na wakazi isipokuwa wakati wa ibada ya Hija.

Masjidul Haram

Mamlaka Kuu ya Takwimu ya Saudi Arabia ilitangaza jana, Ijumaa, kwamba idadi ya Waislamu waliokwenda Makka kuhiji mwaka huu ni mahujaji 899,353, kati yao 779,919 walitoka nje ya Saudia. Idadi ya wanawake ilifikia 412,895.

Mnamo mwaka wa 2019, Waislamu wapatao milioni 2.5 kutoka maeneo mbalimbali ya dunia walishiriki katika ibada ya Hija. Hata hivyo, idadi ya mahujaji ilipungua mwaka 2020 na kufikia elfu 60 tu kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Tags