Jul 10, 2022 08:13 UTC
  • Kanisa la Kiprotestanti la Marekani: Israeli ni dola la ubaguzi wa rangi (apartheid)

Mkutano Mkuu wa Kanisa la Kiprotestanti la Presbyterian la Marekani, huko Louisville, Kentucky, umepiga kura kwa wingi wa asilimia 70 ukiunga mkono azimio la kuitangaza Israeli kama dola la ubaguzi wa rangi.

Uamuzi huo umetajwa kuwa msimamo wa kwanza wa aina hiyo kuchukuliwa na mojawapo ya makanisa makubwa ya Kiprotestanti nchini Marekani.

Uamuzi wa kanisa hilo – ambalo wafuasi wake wanakadiriwa kufikia takriban Wamarekani milioni moja na laki 700 –, unasema kuwa sheria, sera na kanuni za Israel dhidi ya watu wa Palestina zinaendana na maelezo ya kifungu cha sheria ya kimataifa ya ubaguzi wa rangi (apartheid).

Mkutano Mkuu wa Kanisa la Presbyterian (Presbyterian Church) pia uliamua, wakati wa mikutano yake iliyofanyika kwa muda wa siku kadhaa na kuhitimishwa jana Jumamosi, kujumuisha kumbukumbu ya maafa ya watu wa Palestina (Siku ya Nakba) kati ya siku zinazohuishwa na kukumbukwa na kanisa hilo katika kalenda yake.

Vyanzo vya kanisa hilo vimesema kwamba "lobi" na makundi ya mashinikizo yanayofungamana na Israeli yalishinikiza kwa ajili ya kuzuia zoezi la kupiga kura kuhusu maazimio yanayohusiana na Palestina na Israeli.

Uamuzi wa kanisa hilo la Kiprotestanti wa kuitangaza Israel kama dola la ubaguzi wa rangi, umepokewa kwa shangwe na wanaharakati wengi wa Kipalestina, huku makundi yanayoiunga mkono Israel yakiukosoa.

Kwa Wapalestina, tarehe 15 Mei mwaka 1948 ni "Siku ya Nakba" na kielelezo cha kuhamishwa kwa nguvu wananchi hao wanaoendelea kudhulumiwa hadi leo katika makazi yao ya asili. Siku ya Nakba ni kumbukumbu ya masiku machungu ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi za ya Palestina, kuporwa ardhi hiyo; na kwa mara ya kwanza kushuhudiwa wimbi kubwa la Wapalestina laki nane waliofukuzwa na Wazayuni maghasibu kwenye nyumba na makazi yao na kulazimika kuwa wakimbizi.

Tags