Papa aenda Canada kuomba radhi kutokana na jinai za Katoliki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i86192-papa_aenda_canada_kuomba_radhi_kutokana_na_jinai_za_katoliki
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis anatazamiwa kuizuru Canada kesho Jumapili kwenda kuomba radhi kwa wenyeji asilia wa nchi hiyo, kwa dhulma zilizofanyika katika shule za bweni za Wamishonari wa kanisa hilo dhidi ya wenyeji hao.
(last modified 2026-02-02T05:45:46+00:00 )
Jul 23, 2022 11:22 UTC
  • Papa aenda Canada kuomba radhi kutokana na jinai za Katoliki

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis anatazamiwa kuizuru Canada kesho Jumapili kwenda kuomba radhi kwa wenyeji asilia wa nchi hiyo, kwa dhulma zilizofanyika katika shule za bweni za Wamishonari wa kanisa hilo dhidi ya wenyeji hao.

Katika ziara hiyo ya siku tano, Papa anatazamiwa kukutana na kuziomba radhi familia za wahanga wa jinai hizo zilizofanywa dhidi ya watu wa makabila asilia ya Canada.

Papa Francis anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo pia na viongozi wa wenyeji asili wa Canada katika ziara yake hiyo nchini humo.

Kuanzia mwaka 1883 hadi 1996 zaidi ya watoto laki moja na nusu wa wakazi asilia wa Canada walilazimishwa kuishi katika shule makhsusi za bweni zilizokuwa zikisimamiwa na wamishonari na wahubiri wa Kikatoliki. 

Lengo kuu la kutekelezwa mradi huo lilikuwa kuwatenganisha watoto hao na jamii zao asili za Canada ili kuwazuia kujifunza lugha, mila na desturi zao.

Wacanada asilia wakilalamikia jinai dhidi ya watoto

Watoto hao walikumbwa na masaibu chungu nzima ambapo wengi waliteswa, kunajisiwa na kudhalilishwa kingono wakiwa katika shule za wamishonari wa Kikatoliki. Kutokana na hali hiyo baadhi ya watoto walipoteza maisha msimu wa baridi wakiwa jangwani wakijaribu kutoroka hali mbaya shuleni. 

Ripoti ya Kamati ya Ukweli na Maridhiano ya mwaka 2015 imeonyesha kuwa, watoto wasiopungua 4,100 waliuliwa wakiwa katika shule za bweni za Wamishonari wa Kikatoliki au kutoweka. Katika miezi ya hivi karibuni, kumegunduliwa mamia ya makaburi yasiyojulikana na maeneo ilipozikwa miili ya watoto wa wakazi asilia waliokuwa wakishikiliwa katika shule hizo.