Russia yasema itajibu chokochoko zozote tarajiwa za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i95168-russia_yasema_itajibu_chokochoko_zozote_tarajiwa_za_marekani
Kufuatia makabiliano ya kijeshi kati ya Russia na Marekani katika anga ya Bahari Nyeusi Jumanne ya juzi, Wizara ya Ulinzi ya Russia imesisitiza kuwa, taifa hilo litatoa majibu muafaka kwa uchokozi wowote tarajiwa wa Marekani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 16, 2023 09:53 UTC
  • Russia yasema itajibu chokochoko zozote tarajiwa za Marekani

Kufuatia makabiliano ya kijeshi kati ya Russia na Marekani katika anga ya Bahari Nyeusi Jumanne ya juzi, Wizara ya Ulinzi ya Russia imesisitiza kuwa, taifa hilo litatoa majibu muafaka kwa uchokozi wowote tarajiwa wa Marekani.

Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kuwa, Russia haishughulishwi na matukio ya aina hiyo (tukio la droni), lakini haitasita kujibu mapigo kwa chokochoko zote za Marekani dhidi yake.

Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergei Shoigu amemuambia Mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) kuwa, hatua ya Marekani ya kushadidisha ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia mkabala wa Russia ndiyo iliyopelekea kujiri tukio hilo la droni. 

Jumanne asubuhi, ndege ya kivita ya Russia aina ya Sukhoi Su-27 iligongana na ndege isiyo na rubani (droni) ya Marekani aina ya MQ-9 Reaper katika anga ya Bahari Nyeusi, na kupelekea droni hiyo kuanguka kwenye maji ya kimataifa.

Droni ya Marekani

Shoigu amemuambia Lloyd Austin, Mkuu wa Pentagon kuwa, upuuzaji wa sheria za anga ya kimataifa na kuongeza harakati za kiitelijensia dhidi ya maslahi ya Shirikisho la Russia vimesababisha kutokea makabiliano hayo ya kijeshi kati ya Russia na Marekani katika anga ya Bahari Nyeusi.

Uhusiano wa Russia na Marekani umeingia katika mkondo wa mivutano inayoongezeka kila siku hasa kufuatia hatua ya Marekani na washirika wake wa Ulaya ya kuipa Ukraine silaha za kisasa katika vita vyake na Russia.