Mar 30, 2023 07:40 UTC
  • Wanawake wanaovaa Hijabu Austria wakabiliwa na chuki dhidi ya Uislamu

Asasi moja isiyo ya kiserikali imeripoti kuwa, wanawake wanaovaa vazi la staha la Hijabu nchini Austria wanakabiliwa na ongezeko la ubaguzi na hujuma za chuki dhidi ya Uislamu ikilinganishwa na wanaume katika nchi hiyo ya Ulaya.

Munira Mohamud, mwanaharakati wa asasi hiyo ya Austria ya Dokustelle amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa, zaidi ya matukio 1,000 ya chuki dhidi ya Waislamu yaliripotiwa mwaka jana nchini humo, huku wanawake wanaovaa Hijabu wakiwa wahanga wakuu wa kesi hizo.

Maelezo ya kina ya utafiti wa shirika hilo lisilo la kiserikali kuhusu visa vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vilivyosalijiliwa mwaka jana 2022 yanatazamiwa kutolewa mwezi Mei mwaka huu.

Hata hivyo takwimu za asasi hiyo ya Dokustelle zinaonesha kuwa, asilimia  69.2 ya wanawake Waislamu walikabiliwa na hujuma za kibaguzi na chuki kutokana na imani yao mwaka 2021.

Mohamud, mkazi wa Vienna, na mmoja wa wanawake Waislamu walioshambuliwa kwa kuvaa Hijabu mwaka jana anasema, "Mwanamme mmoja alinikabili nilipokuwa nje, akaniliuza, nini hii umevaa kichwani, ivue!"

Austria, kitovu kipya cha ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu barani Ulaya

Hata hivyo, sio uhalifu wa mitaani pekee unaotekelezwa, ambao unawalenga Waislamu. Mvutano mkali wa 2021 ulidaiwa kuchochewa na serikali yenye utata iliyotekeleza "Ramani ya Uislamu," iliyoanzishwa na mamlaka ili kufanya upelekelezi na ujasusi katika misikiti yote kote Austria. Wakosoaji wanaamini kuwa sera hii ilichangia kuchochea  kuenea kwa uhalifu wa chuki dhidi ya Uislamu.

Aidha Novemba 2020, mamlaka ya Austria ilizindua Oparesheni Luxor, ambayo ilishuhudia nyumba na ofisi za mashirika ya kutoa misaada ya Kiislamu na wanaharakati zikivamiwa kama sehemu ya kile kinachoitwa vita dhidi ya "Uislamu wa kisiasa." Kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali ya Austria, kuna Waislamu wapatao 645,600 katika nchi hiyo ya Ulaya. 

 

Tags