May 09, 2023 01:23 UTC
  • Jibu na hatua za serikali ya India dhidi ya uasi uliozuka katika majimbo manane ya nchi hiyo

Uasi katika jimbo la Manipur umeilazimisha serikali ya India kutuma vikosi vya uchukuaji hatua za haraka na kuweka marufuku ya kutotoka nje katika miji minane tofauti ya nchi hiyo.

Kutokana na hali kuwa mbaya zaidi, serikali ya New Delhi imeomba msaada wa jeshi ili kutuliza hali hiyo. Wakati vikitangaza amri ya kutotoka nje katika miji ya jimbo la Manipur lililoko kaskazini mashariki mwa India, vikosi vya jeshi vimeanza kushika doria mitaani kwa lengo la kusitisha mapigano hayo.
Mapigano na machafuko ya kikabila katika jimbo la Manipur kaskazini mashariki mwa India yamesababisha vifo vya watu 54 ndani ya kipindi cha siku chache zilizopita. Mbali na maafa ya roho za watu, machafuko hayo yamesababisha hasara kubwa pia za kiuchumi kwa watu na taasisi za serikali.
Kuhusiana na hali hiyo Birn Singh, afisa wa ngazi ya juu kabisa katika jimbo la Manipur amesema, katika mapigano na machafuko yaliyoanza Jumatano iliyopita katika jimbo hilo lililoko karibu na mpaka wa Myanmar, makanisa kadhaa yamebomolewa na nyumba na magari kadhaa yameharibiwa.

Machafuko na mapigano ya kikabila yaliyozuka katika jimbo la Manipur kaskazini mashariki mwa India, yalianza Jumatano iliyopita baada ya maandamano ya upinzani yaliyofanywa na kundi moja la raia kugeuka fujo na ghasia kufuatia uingiliaji kati wa Polisi. Mapigano hayo, kwanza yaliibuka katika mji wa Churachandpur ulioko kwenye jimbo la Manipur, sambamba na maandamano ya watu elfu kumi yaliyoongozwa na jamii ya Kuki na makabila mengine ya Kikristo. Ukweli ni kuwa, maandamano hayo yalifanywa dhidi ya jamii za Wahindu, ambazo zinataka zipewe upendeleo zaidi kulinganisha na makabila mengine. Wahindu wanataka wawe na haki ya kulima katika mashamba ya misitu, kupatiwa mikopo yenye masharti nafuu zaidi, mgawo mkubwa zaidi wa nafasi za ajira na suhula za uhakika zaidi za matibabu na elimu.

Waandamanaji wanahisi jamii za Kihindu katika jimbo la Manipur zina hali nzuri ikilinganishwa na jamii zingine. Ndiyo maana wanalitafsiri suala la kuwapatia Wahindu upendeleo mkubwa zaidi kuwa ni hatua ya kuongeza ubaguzi na upendeleo katika jimbo hilo. Na hii ni katika hali ambayo, asilimia nane ya jumla ya wakazi wote wa Manipur yenye watu milioni 2.5 ni Waislamu. Kabla ya hapo, baadhi ya wataalamu na wadadisi wa masuala ya ndani ya majimbo ya India walieleza kwamba, kwa mtazamo wao, matatizo ya kimaisha ndio sababu kuu ya maandamano ya upinzani yanayofanywa na watu wa jamii za wasiokuwa Wahindu.
Hali ni tete katika jimbo la Manipur

Kuhusiana na hilo, Havid Marwa, mkuu wa zamani wa Polisi ya India na mtaalamu na mweledi wa masuala ya majimbo katika nchi hiyo yenye idadi kubwa ya watu amesisitiza kuwa "serikali ya Delhi inapaswa ifanye jitihada zaidi za kuboresha hali ya kiuchumi na ya maisha ya watu". Katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la IRNA huko New Delhi, Marwa amesema: "ili kukomesha machafuko katika majimbo kama Manipur, serikali kuu ya India inapaswa kuwa na ushirikiano zaidi na majimbo haya."

Ukweli huu haupaswi kupuuzwa, kwamba India, ikiwa sasa ni nchi yenye watu wengi zaidi duniani, imeundwa na  jamii za makabila tofauti. Kwa sababu hiyo, migogoro ya kikabila katika nchi hiyo yenye watu wengi ina historia ndefu. Kulingana na takwimu zilizochapishwa na vyombo vya habari vya India, kuanzia muongo wa 1950 hadi sasa, watu wasiopungua 50,000 wamepoteza maisha katika mizozo na mapigano ya kikabila na ya kupigania kujitenga yaliyotokea katika jimbo la Manipur.
Licha ya matukio yote yaliyojiri huko nyuma, lisilo na shaka ni kuwa kutwaa hatamu za madaraka na wadhifa wa uwaziri mkuu Narendra Modi kumeshadidisha na kukoleza moto wa mizozo na tofauti za kikabila nchini India. Na bila shaka yoyote, Waislamu ndio wahanga na waathirika wakuu wa upendeleo na ubaguzi huo wa mbari. Lakini si Waislamu peke yao ambao ni waathirika wa utendaji wa viongozi wa serikali ya Kihindu. Wakristo na Wayahudi, nao pia hivi karibuni wameingia kwenye makabiliano na mapigano na jamii za Wahindu. Ukubwa wa machafuko na mapigano umefikia hadi ya kuifanya serikali ya New Delhi ilazimike kutoa amri ya jeshi kuingilia kati ili kukomesha mapigano na makabiliano hayo.
Narendra Modi

Kuwepo kwa mizozo na mapigano ya kikabila iliyotokana na sera ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja ya serikali ya Narendra Modi kuhusiana na makabila na jamii tofauti za watu wa India imezifanya baadhi ya jamii hizo zikate tamaa na kupoteza matumaini kwa serikali ya New Delhi na badala yake kuchukua hatua za kuanzisha mapambano ya mtutu wa bunduki. Hatua hiyo ya kuamua kubeba silaha imelipatia kisingizio kizuri jeshi la India cha kupambana na wapinzani linaowatambulisha kama 'magaidi'.

Kwa mujibu wa mashirika ya Intelijensia ya India, magaidi hao wanapanga kuvuruga amani kabla ya mkutano wa G20 uliopangwa kufanyika Srinagar mwishoni mwa mwezi huu. Baada ya kupokea taarifa kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi dhidi ya magari na mitambo ya kijeshi, Jeshi la India limetoa amri kwa magari ya kijeshi kutosimama masokoni na kuendelea kufungwa skuli ya Jeshi iliyoko katika mji wa Sonjawan.../

 

Tags