Mar 18, 2024 11:12 UTC
  • Wanafunzi wa kigeni washambuliwa India kwa kusali Tarawehe kwenye dakhalia ya chuo

Wanafunzi wasiopungua wanne wa kigeni wamejeruhiwa baada ya kundi la Wahindu wenye chuki za kidini kuvamia dakhalia ya chuo kikuu katika jimbo la Gujarat magharibi mwa India na kushambulia kundi la wanafunzi waliokuwa wanasali Sala ya Tarawehe katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Wanafunzi walioshambuliwa wamevieleza vyombo vya habari vya ndani kuwa kikundi kidogo kilikusanyika Jumamosi usiku ndani ya majengo ya dakhalia ya wavulana kwa ajili ya Sala ya Tarawehe kwa kuwa hakuna msikiti kwenye chuo kikuu kilichoko Ahmedabad. Muda mfupi baadaye, kundi la watu waliokuwa na fimbo na visu walivamia hosteli hiyo na kuwashambulia wanafunzi hao na kufanya uharibifu ndani ya vyumba vyao.

Mwanafunzi mmoja amesema: "kikundi cha wanafunzi 15 walikuwa wanasali wakati watu watatu walipowajia na kuanza kupiga makelele ya 'Jai Shri Ram' yaani [Salamu bwana Ram]. Walituzuia tusisali hapa”.

Uharibifu uliofanywa kwenye vyumba vya wanafunzi Waislamu

Mwanafunzi huyo ameendelea kueleza kwamba, baada ya muda, watu wapatao 250 walijitokeza na kuanza kupiga makelele ya 'Jai Shri Ram' na kuwapiga mawe na kuharibu mali za hosteli.

Mwanafunzi kutoka Afghanistan ameiambia televisheni ya NDTV: "walitushambulia ndani ya vyumba pia. Walivunja laptopu, simu na baiskeli zilizoharibika”.

Mwanafunzi mmoja kutoka Afrika amesema: "hatuwezi kuishi hivi, tulikuja India kusoma na sasa tunashambuliwa kwa sababu ni wakati wa Ramadhani na kwa sababu Waislamu wanasali".

Tovuti ya habari ya Indian Express imeripoti kuwa wanafunzi wawili walijeruhiwa vibaya na wanaendelea kupata matibabu hospitalini baada ya wanafunzi kutoka Afghanistan, Uzbekistan, Sri Lanka, Bangladesh na nchi kadhaa za Afrika kushambuliwa.

Makundi ya Wahindu ya mrengo wa kulia yenye misimamo mikali na chuki za kidini yamekuwa yakiendesha kampeni za hujuma na mashambulio katika maeneo ya umma dhidi ya Waislamu wanaosali.

Mapema mwezi huu, askari polisi mmoja katika mji mkuu New Delhi alisimamishwa kazi baada ya kuwapiga mateke wanaume Waislamu waliokuwa wakisali kando ya barabara.../

Tags