May 14, 2023 11:44 UTC
  • Waturuki wapiga kura katika uchaguzi muhimu zaidi tangu wa mwanzo wa vyama vingi 1950

Upigaji kura katika uchaguzi wa 13 wa urais na wa 28 wa wabunge nchini Uturuki ulianza leo saa mbili asubuhi nchini kote na ulitazamiwa kuendelea hadi saa 11 jioni kwa saa za nchi hiyo.

Katika uchaguzi huo, watu milioni 60,697,843 wametimiza masharti ya kupiga kura ambapo kati ya hao, 4,904,672 wameshiriki katika upigaji kura kwa mara ya kwanza. Aidha kuna wafungwa 53,171 ambao walitazamiwa kupiga kura wakiwa magerezani.

Kwa kujiengua Muharrem İnce, kiongozi na mgombea wa chama cha Ardhi ya Nyumbani (Homeland), Recep Tayyip Erdogan, mgombea wa muungano wa Jamhuri, Kemal Kilicdaroglu, aliyegombea kwa tiketi ya muungano wa Taifa, na Sinan Oğan, mgombea wa muungano wa ATA, ndio waliochuana katika kinyang'anyiro cha urais.

Aidha vyama 24 na wagombea binafsi 151 wameshiriki katika uchaguzi wa kugombea viti katika Bunge la Uturuki lenye jumla ya viti 600.

Uchaguzi wa leo umetajwa kuwa ama fursa ya kurefushwa au kuhitimishwa utawala wa miongo miwili wa Erdogan ambapo hivi sasa uko kwenye mfumo wa urais au kurejeshwa mfumo wa bunge kama ilivyoahidiwa na mrengo wa upinzani.

Uchaguzi wa rais na bunge uliofanyika leo nchini Uturuuki umeelezewa na wengi kuwa muhimu zaidi tangu nchi hiyo ilipofanya uchaguzi wake wa kwanza huru katika mfumo wa vyama vingi katika tarehe kama ya leo pia ya Mei 14, mwaka 1950.

Waturuki wameelekea kwenye vituo vya kupigia kura leo wakati nchi yao inashuhudia hali mbaya ya kupanda kwa gharama za maisha baada ya mfumuko wa bei kufikia asilimia 85 mwezi Oktoba mwaka jana sambamba na matetemeko makubwa ya ardhi yaliyotokea mwezi Februari, ambayo yaliua zaidi ya watu 50,000.

Tume ya uchaguzi ya Uturuki imetangaza kuwa matoeko ya awali yataanza kutolewa leo mnamo saa 5 na dakika 59 usiku.../

Tags