Jun 05, 2023 02:35 UTC
  • US yahamakishwa na muungano wa baharini wa Iran, Saudia, nchi za Ghuba ya Uajemi

Jeshi la Baharini la Marekani limetiwa kiwewe na tangazo la Iran la kutaka kuundwa muungano wa vikosi vya baharini vya Jamhuri ya Kiislamu, Saudi Arabia na nchi nyingine za Ghuba ya Uajemi.

Msemaji wa Kikosi cha Tano cha Jeshi la Marekani, Kamanda Tim Hawkins amenukuliwa na tovuti vya Breaking Defense akisema kuwa, "Nukta kwamba Tehran karibuni itaunda muungano wa kijeshi wa baharini na Saudia na nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi inakwenda kinyume na mantiki."

Mbali na matamshi hayo, Hawkins amekariri bwabwaja na madai ya kukaririwa ya huko nyuma ya Washigton eti kwamba Iran inahatarisha usalama wa maji ya kieneo kwa mienendo yake.

Ijumaa iliyopita, Admeli Shahram Irani, Kamanda wa Vikosi vya Majini vya Iran alitangaza kuwa, Majeshi ya Baharini ya Iran na nchi nyingine za Asia Magharibi kama Saudi Arabia, Imarati, Qatar, Bahrain na Iraq karibuni yataunda muungano wa pamoja.

Askari vamizi wa US  katika maji ya eneo la Ghuba ya Uajemi

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, uwepo wa vikosi ajinabi hapa Asia Magharibi umekuwa na taathira hasi kwa amani na usalama wa eneo hili, na kwamba nchi za eneo hili zina uwezo wa kujidhaminia usalama wao.

Hivi karibuni, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ulitangaza kujiondoa kwenye Muungano wa Vikosi Vya Baharini wenye makao makuu Bahrain. Makao hayo yako karibu na Kikosi cha Tano cha Manowari za Marekani na Kamandi Kuu ya nchi hiyo. 

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kujitoa Imarati katika Muungano wa Baharini unaoongozwa na Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati ni ushahidi wa wazi wa kupungua ushawishi wa Washington si tu katika eneo, bali kote duniani.

Tags