China na Palestina zaafikiana kuanzisha ushirikiano wa kistratajia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i98800-china_na_palestina_zaafikiana_kuanzisha_ushirikiano_wa_kistratajia
Rais Xi Jinping wa China amekutana na kufanya mazungumzo na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mjini Beijing, ambapo wawili hao wameafikiana juu ya kuanzisha ushirikiano wa kistratajia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2023 03:04 UTC
  • China na Palestina zaafikiana kuanzisha ushirikiano wa kistratajia

Rais Xi Jinping wa China amekutana na kufanya mazungumzo na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mjini Beijing, ambapo wawili hao wameafikiana juu ya kuanzisha ushirikiano wa kistratajia.

Katika mkutano huo wa jana Jumatano, Rais Xi amesema ushirikiano huo utaimarisha uhusiano wa pande mbili, katika misingi ya mafanikio ya huko nyuma na kufungua ukurasa mpya kwa ajili ya mustakabali wa mataifa hayo.

Rais wa China amebainisha kuwa, "China na Palestina zitashirikiana kuimarisha urafiki na ushirikiano wao katika nyuga zote, kwa kuwa watu wa nchi mbili hizi ni marafiki wa karibu, tena wanaoaminiana."

Amesisitiza kuwa, Beijing itaendelea kuunga mkono mapambano halali ya Wapalestina ya kupigania haki zao za kitaifa, na kuongeza kwamba ukandamizaji wa kihistoria wanaofanyiwa watu wa Palestina haupaswi kuendelea kwa muda usiojulikana. 

Rais Xi Jingpin wa China ameeleza bayana kuwa, haki halali, za msingi na za kitaifa za Wapalestina hazipaswi kuendelea kupuuzwa.

Rais Xi amesema China itaendelea kuiunga mkono Palestina hadi pale itakapopewa uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa, sanjari na kuendelea kulitetea taifa hilo la Kiarabu katika majukwaa ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Wang Wenbin, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, China na Palestina zina uhusiano wa kidugu wa jadi, na kuwa hatua ya China kuwa mwenyeji wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina inaashiria urafiki wa karibu baina ya Wachina na Wapalestina.