Mapinduzi ya Kiislamu na moyo wa kujiamini
Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya makala hizi maalumu zinazokujieni kwa mnasaba wa siku hizi za kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Ni matumaini yetu kwamba mtaendelea kuwa kando ye redio zenu kusikiliza tuliyokuandalieni.
Siku hizi wapenzi wasikiliji ni siku za shangwe, furaha na vifijo kwa taifa la Iran. Siku hizi zinakumbusha ushindi wa thamani wa wananchi waliokuwa mikono mitupu dhidi ya utawala uliokuwa umejizatiti kwa silaha za kisasa ukiungwa mkono na kusaidiwa na madola yote makubwa duniani. Tofauti na mapinduzi mengine makubwa yaliyotokea duniani, furaha na tamu ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran bado inahisika hadi hii leo licha ya kupita karibu miongo minne sasa tangu yapate ushindi. Kiongozi wa Mapinduzi hayo hayati Imam Ruhullah Khomeini amesema: "Siri kubwa ya ushindi wa Mapinduzi haya ni imani kubwa ya taifa la Iran kwa Mwenyezi Mungu Muweza na umoja na mshikamano wa wananchi." Tangu mwanzoni mwa mapambano yake, Imam alikuwa akisisitiza kuwa harakati hiyo si dhidi ya utawala wa kifalme nchini Iran pekee bali ni mapambano ya Uislamu dhidi ya madola yote ya kibeberu ya mashariki na magharibi.
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliwashangaza na kuwaacha bumbuazi wasomi na wanafikra wengi duniani. Wanasiasa duniani hawakuweza kuamini kwamba wananchi walioshi chini ya ukandamizaji mkubwa kwa miaka mingi na kupoteza matumaini na uwezo wa kujiamini kutokana na siasa za kikoloni za mabeberu wangeweza- kwa uongozi wa mzee aliyekuwa na umri wa miaka zaidi ya 70- kukunja jamvi la utawala uliokuwa ukiungwa mkono na madola yote makubwa. Wachambuzi wengi walishangazwa sana na hali ya kujiamini kukubwa kwa taifa la Iran wakati wa harakati za mapinduzi. Gazeti la Times la Uingereza licha ya misimamo yake iliyokuwa dhidi ya harakati za wananchi Waislamu wa Iran, pia lilishindwa kuficha mshangao wake kutokana na kujiamini kwa taifa la Ian. Gazeti hilo la Times liliandika kuwa: Imam Khomeini alikuwa mtu aliyeweza kuwaathiri watu wengi kwa maneno yake. Alikuwa akizungumza kwa lugha nyepesi na ya watu wa kawaida na kuwapa moyo wa kujiamini na matumaini wafuasi wake maskini na waliokuwa wakikandamizwa. Hisia hii iliwawezesha Wairani kumfutilia mbali kila mtu aliyesimama mkabala wao. Khomeini aliwaonesha wananchi wa Iran kwamba, wanaweza kupambana bila woga na madola makubwa kama Marekani", mwisho wa kunukuu.
Hali ya kujiamini kwa taifa ni jambo lenye uhusiano wa aina mbili na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Kwani kwa upande mmoja hali hiyo ilikuwa sababu ya ushindi wa taifa la Iran, na wakati huo huo ni miongoni mwa matunda ya mapinduzi hayo. Mwanzoni kabisa mwa mapambano yake, Imam Khomeini aliwakumbusha Wairani neema na uwezo mkubwa waliopewa na Mwenyezi Mungu. Daima alikuwa wakiwakumbusha wananchi kwamba, mabebebru wanatumia mbinu mbalimbali na propaganda za uongo kwa ajili ya kulibakisha nyuma taifa la Iran na kulifanya liamini kwamba haliwezi kifanya lolote katika medani za sayansi na teknolojia, elimu na utawala, lakini sisi tunaweza kuainisha mustakbali wetu kwa kutumia azma na irada yetu madhubuti na kufidia kipindi cha kubakia nyuma kimaendeleo. Imam Khomeini alisema: Moja kati ya masaibu makubwa yaliyosababishwa na mabeberu kwa taifa letu ni kwamba walilifanya taifa lijishuku na kupoteza hali ya kujiamini.. Walitumia propaganda kwa ajili ya kutufanya tuwe na dhana mbaya kuhusu nafsi zetu sisi wenyewe na kwa utaratibu huo tukapoteza hali ya kujiamini.." mwisho wa kunukuu.
Kujiamini ni miongoni mwa nguzo muhimu za shakhsia ya mtu binafsi na jamii na sababu muhimu inayoiwezesha jamii, taifa na nchi kufika kwenye kilele cha izza na mafanikio. Kuwepo kwa sifa hiyo huwa sababu ya maendeleo na ukamilifu na kukosekana kwake huwa sababu ya kudhalilishwa, kudunishwa na kutawaliwa na mabeberu na wageni. Kujiamini kwa taifa kuna maana ya kuwa na imani kuhusu uwezo na vipawa vya taifa husika. Kila taifa lina vipawa na uwezo ambao pale taifa husika linapoutambua na kuutumiwa ipasavyo, huwa na sifa hii ya kujiamini kitaifa. Kuwa na hali ya juu kabisa ya kujiamini kunakozidisha uwezo wa mtu wa kupambana na matatizo mbalimbali hupatikana chini ya kivuli cha kumwamini na kumtegemea Mwenyezi Mungu, kwani chini ya kivuli cha kumtegemea Mola Muweza, mwanadamu huwa hajihisi tena kuwa yu mpweke bali hujiona kuwa yuko pamoja na Mwenyezi Mungu Muweza wakati wote. Imam Khomeini aliamsha na kuchochea imani ya kidini ya wananchi wa Iran na hivyo kuamcha na kuhuisha hali ya kujiamini katika nafsi zao. >>>
Miongoni mwa vizuizi vya hali ya kujiamini ni kuwafanya watu wasijue uwezo wao na wa taifa lao. Kabla ya ushidi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini serikali tegemezi zikishirikiana na wakoloni wa Kimagharibi, daima zilikuwa zikifanya jitihada za kuwafanya wananchi wasitambue uwezo na vipawa vyao. Siasa na sera hiyo ya nchi za Magharibi ilitumiwa na ingali inatumiwa na wakoloni wa Kimagharibi dhidi ya Iran na mataifa mengine duniani. Wakoloni hao walikuwa wakidharau na kudunisha uwezo na vipawa vya vijana Waislamu wa Iran na matokeo yake ni kuwa, katika kila suala la kitaalamu Wairani walitumikishwa kama vibarua tu au wasaidizi wa wataalamu kutoka Marekani na nchi za Ulaya. Hali hiyo ilishuhudiwa hata katika masuala kama ya jenzi wa mabwawa, njia za chini kwa chini, utengenezaji na ukarabati wa mashine za viwandani na kadhalika. Vipuri vya ndege vilikuwa vitumwa Marekani kwa ajili ya kutengenezwa na kijana wa Iran hakuwa na haki ya kujifunza au kuingia katika masuala kama hayo. Sera hizo ziliyeyusha hali ya kujiamini katika nafsi za Wairani kiasi kwamba waliamini kuwa, hawawezi kufanya kazi na mambo mengi yanayofanywa na watu wa Magharibi.
Utawala wa nchi na uendeshaji wa masuala ya kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi pia ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo kutokana na siasa za kikoloni, wananchi wa Iran walijihisi kwamba hawayawezi. Marekani na Uingereza zilikuwa zikiainisha au kuuzulu serikali nchini Iran kirahisi na wananchi hawakuwa na nafasi yoyote katika mambo hayo. Serikali hizo tegemezi zilikuwa zikihudumia maslahi ya nchi zinazoziunga mkono badala ya kushughulikia maslahi na matakwa ya wananchi; hivyo Wairani walikuwa wakipata taabu na mashaka siku baada ya siku na kutwishwa hali ya udhalili na unyonge wa kuwa taifa tegemezi. Imam Khomeini alisimama kidete na kwa ushujaa kupambana na hali hiyo na akaanza kuwazindua wananchi kuhusu uwezo wao wa kidini na kitaifa. Kwa msingi huo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu taifa la Waislamu wa Iran liliamini uwezo wake, azma yake kubwa na hazina yake adhimu ya kidini na kitaifa. Tangu wakati huo taifa liliingia katika medani mbalimbali za elimu na teknolojia na kupata mafanikio makubwa. Miongoni mwa mafanikio hayo makubwa ni kuendesha masuala ya nchi yao wenyewe bila ya kuingiliwa na wageni au madola makubwa ya kibeberu.
Matunda mengine ya kujiamini kwa taifa la Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ni maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Hivi sasa na kwa hima ya vijana na wasomi wa Iran, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inashika nafasi ya nne katika orodha ya nchi zinazostawi kwa kasi kielimu na kisayanasi duniani na nafasi ya 15 katika kuzalisha elimu. Maendeleo makubwa ya Iran katika teknolojia ya nyuklia, uzalishaji wa makala nyingi za kielimu, maendeleo ya Iran katika sayansi za anga za mbali, mafanikio ya wataalamu wa Iran katika teknolojia ya nano na seli shina ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuashiriwa katika uwanja huu.
Kiongozi wa sawa wa Mapinduzi ya Kiislamu ayatullah Ali Khamenei ameashiria udharura wa kulindwa hali ya kujiamini ndani ya taifa la Iran na mataifa mengine ya Waislamu na yanayokandamizwa duniani na kusema: Kaulimbiu ya "Sisi Tunaweza" alitufunza kiongozi wetu kipenzi Ruhullah Khomeini, na Mapinduzi yametupa ujasiri wa kusema 'sisi tunaweza'. Anaendelea kusema kuwa: Licha ya njama kubwa zinazofanywa na maadui lakini taifa la Iran katika kipindi chote cha miaka iliyopita baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu limewathibitishia maadui na walimwengu wote kwamba "Sisi Tunaweza". >>
Wasikilizaji wapenzi muda wa makala hii umemalizika. Asanteni kwa kuwa nami hadi wakati huu na kwaherini.