Jul 20, 2023 02:39 UTC
  • Leo katika Historia, Alkhamisi 20 Julai

Leo ni Alkhamisi tarehe Pili Mfunguo Nne Muharram 1445 Hijria sawa na Julai 20 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita yaani tarehe Pili Muharram mwaka 61 Hijria, Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na familia na masahaba zake waliwasili katika ardhi ya Karbala katika Iraq ya leo. Miezi kadhaa kabla ya hapo, Imam Hussein AS aliondoka katika mji mtakatifu wa Madina na kuelekea Makka akilalamikia utawala wa kimabavu wa Yazid bin Muawiya na baadaye akaelekea katika mji wa Kufa huko Iraq. Japokuwa watu wa Kufa mwanzoni waliunga mkono mapambano ya Imam Hussein na kumwalika katika mji huo, lakini waliacha kumuunga mkono mjukuu huyo wa Mtume kutokana na hofu na vitisho vya utawala wa Yazid bin Muawiya. Jeshi la Yazidi mlaaniwa liliuzuia msafara wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) kuingia katika mji wa Kufa na kuzingirwa katika jangwa na Karbala. 

Miaka 213 iliyopita katika siku kama ya leo, uhuru wa Colombia ulitangazwa rasmi. Colombia iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 na Wahispania na kuanza kukoloniwa. Kuanzia mwishoni mwa karne ya 18, harakati za kupigania uhuru za wananchi wa nchi hiyo ziliongezeka na hatimaye harakati hizo kuzaa matunda katika siku kama ya leo. Hatua ya Napoleon Bonaparte ya kuikalia kwa mabavu Uhispania, ilizipatia fursa nzuri nchi makoloni ya Uhispania ikiwemo Colombia kuzidisha mapambano ya ukombozi.   

Bendera ya Colombia

Katika siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, Georg Friedrich Bernhard Riemann, mwanahisabati wa Kijerumani aliaga dunia baada ya kuugua maradhi ya kifua kikuu. Georg Friedrich alizaliwa mwaka 1826 katika mji wa Hanover nchini Ujerumani na baada ya kumaliza masomo yake ya awali aliendelea na masomo ya hisabati. Alipofikisha umri wa miaka 28 Bernard Riemann alikuwa tayari ni mhadhiri wa Chuo Kikuu katika uwanja huo wa hisabati.

Georg Friedrich Bernhard Riemann

Miaka 86 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Guglielmo Marconi mvumbuzi wa radio wa Kiitalia akiwa na umri wa miaka 63. Guglielmo alizaliwa mwaka 1874 huku akiwa mtoto wa mfanyabiashara mmoja wa Kiitalia. Marconi alipenda sana kujifunza masuala ya ufundi na sanaa tangu akiwa kijana  mdogo ambapo alianza utafiti wa mawimbi ya sauti. Marconi hatimaye alifanikiwa kuvumbua radio baada ya utafiti wake huo na baadaye akaikamilisha bila ya kutumia waya.   

Guglielmo Marconi

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika mwezini. Katika siku hiyo wanaanga wa Kimarekani Neil Armstrong na Edwin Aldrin walitumia chombo cha kusafiria katika anga za mbali kwa jina la Apolo- 11 na kufika mwezini na baadaye wakarejea duniani huku wakiwa na sampuli za mawe na udongo walizokuja nazo katika safari hiyo. Kwa utaratibu huo juhudi kubwa za mwanadamu zilizokuwa zikifanywa kwa muda mrefu kwa lengo la kufikia mwezini zikawa zimezaa matunda.   

Neil Armstrong

Na miaka 49 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi wa Uturuki walivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Cyprus, mashariki mwa kisiwa hicho. Tangu kale Waturuki na Wagiriki wa Cyprus walikuwa wakizozana juu ya namna gani pande mbili hizo zigawane mamlaka ya nchi hiyo. 

Cyprus

 

Tags