Jumatatu, Juni 27, 2016
Leo ni Jumatatu tarehe 21 Ramadhani 1437 Hijria sawa na 27 Juni 2016 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1397 iliyopita Ali bin Abi Talib (as) Khalifa wa baada ya Mtume Muhammad (saw) na mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume alikufa shahidi. Siku mbili kabla ya hapo Imam Ali (as) alielekea msikitini kwa ajili ya Sala ya asubuhi na akiwa katika sijda alipigwa upanga kichwani na Ibn Muljim aliyekuwa mfuasi wa tapo la Khawarij na kumpasua utosini. Imam Ali (as) alikufa shahidi katika siku kama ya leo na hivyo kufikia saada aliyokuwa akiitaraji daima, yaani kufa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kuuliwa shahidi Imam Ali (as) kulisababisha pigo na msiba usioweza kusahaulika na kufutika kwa Uislamu na Waislamu.
Tarehe 21 Ramadhani miaka 333 iliyopita alifariki dunia faqihi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Abu Jaafar Muhammad bin Hassan maarufu kwa jina la Sheikh Hurr al Aamili huko Jabar Amil nchini Lebanon. Alitokea kuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa kufanya uchunguzi mkubwa. Sheikh Hurr al Amili ameandika vitabu vingi vya fiqhi na hadithi na miongoni mwao ni kile cha Wasaailu Shia ambacho kina nafasi maalumu katika duru za elimu ya fiqhi.
Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, mji wa Sardasht huko magharibi mwa Iran ulishambuliwa kwa mabomu ya kemikali na ndege za kivita za utawala wa zamani wa Iraq. Wakazi wa mji huo wapatao 110 waliuawa shahidi na wengine 530 kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo. Utawala wa zamani wa Iraq ambao ulikuwa umepoteza matumini ya kushinda vita ilivyovianzisha dhidi ya Iran, ulidhani kwamba kwa kuendesha mashambulio ya silaha za kemikali ungeweza kuitwisha Iran matakwa yake kupitia mashambulio hayo ya kinyama, lakini haukufanikiwa kufikia lengo hilo.