Aug 12, 2023 04:48 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (75)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili tuweze kwa pamoja kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.

Katika muendelezo wa kuwatambulisha Maulamaa wa Kishia wa karne ya 14 Hijria, sehemu ya 75 ya mfululizo wetu juma hili, itamtambulisha na kumzungumzia Sheikh Abbas Qummi, mmoja wa wanazuoni watajika na mwandishi wa kitabu mashuhuri cha dua cha Mafatihul-Jinan (Funguo za Pepo). Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

"Qom" ni moja ya miji mikongwe na maarufu ya Iran. Tangu zama za kale, mji huu umekuwa miongoni mwa miji ya kidini na muhimu ya Iran kutokana na kuwepo kwa Haram ya Bibi Fatma Maasuma (as), ambaye ni binti ya Imam Musa al-Kadhim (as) na dada yake Imam Ridha (as). Maulamaa na shakhsia wengi wakubwa wamesoma katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) kinachopatikana katika mji huo, chuo ambacho ni moja ya ngome muhimu za kielimu katika Ulimwerngu wa Kiislamu. Baadhi ya wanazuoni hawa wamekuwa na athari kubwa sana katika historia ya madhehebu ya Shia, au wametoa zawadi kwa ulimwengu wa Kiislamu kutokana na taathira na athari zao kubwa za kielimu na kidini ambazo ni maalumu na ambazo wamevirithisha vizazi vilivyokuja baada yao.

Haram ya Bibi Fatma Maasuma (as), Qom, Iran

 

Mwishoni mwa karne ya 13 Hijria, alikuwa akiisha mfanyabiashara mmoja katika mji wa Qom ambaye aliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Haj Muhammad Reza Qummi. Licha ya kuwa, bwana huyu alikuwa miongoni mwa watu wa tabaka la wafanyabiashara lakini alikuwa na maarifa na elimu kubwa sana kuhusu dini, kiasi kwamba, akthari ya watu wa mji wa Qum walikuwa wakimrejea kwa ajili ya kujifunza maarifa, elimu na sheria za dini. Mwaka 1294 Hijria, al-Haj Muhammad Reza Qummi aliruzukiwa mtoto wa kiume ambaye alimpa jina la Abbas.  Mtoto Abbas alikipitisha kipindi cha utoto wake katika anga iliyojaa imani na kushikamana na dini kutokana na wazazi wake kuwa wacha Mungu na watu walioshikamana barabara na dini. Mama yake aliyejulikana kwa jina la Zaynab, alikuwa mwanamke mwema, mtakasifu na aliyeshikamana na dini kikamilifu huku akiwa amepambika kwa sifa njema za kimaadili.

Sheikh Abbas Qummi mwandishi wa kitabu cha Mafatihul-Jinan tunayemzungumzia leo anaamini kwamba, mafanikio yake ni natija ya zuhdi (kuipa mgongo dunia) na uchaji Mungu wa mama yake. Katika kipindi cha ubarobaro wake, Abbas alisoma kwa baba yake na kwa mmoja wa walimu mahiri wa Hawza ya Qum na mwaka 1316 Hijria akiwa na umri wa miaka 20 alifunga safari na kuelekea Najaf Iraq, kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Sheikh Abbas Qummi akiwa kijana aliondokea kupenda mno elimu ya kuwajua wapokezi wa hadithi na kunukuu hadithi za Ahlul-Bayt (as). Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana alipofika Najaf alivutiwa sana na darsa za masomo ya Mirza Hussein Nuri, mpokezi mkubwa wa hadithi.

Shekhe Nuri

 

 

 

Akiwa huko Najaf, Sheikh Abbas Qummi, alifanya hima kubwa ya kujifunza kwa Mirza Hussein Nuri. Alihudhuria masomo ya Muhaddith Nuri kwa muda wa miaka minne na katika kipindi hiki juhudi zake zilifikia kiwango ambacho alichukuliwa kuwa miongoni mwa wanafunzi wa daraja la kwanza wa mwalimu huyu. Baada ya kifo cha mwalimu wake, mwaka 1322 Hijria mwafaka na 1904, Sheikh Abbas Qummi alirejea Qom akiwa amebeba mzigo mkubwa wenye thamani wa elimu na maarifa. Ni katika kipindi hiki ambapo Sheikh Abbas Qummi alianza kufundisha na kuandika vitabu. Kipindi fulani aliishi katika mji wa Mash’had na alifanya kazi kubwa ya kutoa mihadhara, kufundisha na kualifu vitabu kiasi kwamba, alikuwa mashuhuri na msomi mtajika miongoni mwa watu wa matabaka yote. Katika hotuba zake, Sheikh Abbas Qummi alikuwa akifanya ufichuaji dhidi ya mambo yasiyofaa na kuwaeleza masuala muhimu ya zama zao yanayohusiana na jamii. Hali hiyo ilimfanya mara kadhaa akabiliwe na vitisho kwa kuuawa na wapinzani na vibaraka wa utawala uliokuwa madarakani.

Katika zama hizi, Reza Shah, mfalme wa kwanza wa ukoo wa Kipahlavi alikuwa ameingia madarakani nchini Iran kwa himaya na uungaji mkono wa Uingereza. Reza Shah ambaye alikuwa na mapenzi makubwa na utamaduni na ustaarabu wa Kimagharibi, alikusudia kufanya mabadiliko katika utamaduni wa wananchi wa Iran na alianza kulifanyia kazi hilo na kubadilisha mavazi ya watu. Hata hivyo Maulamaa walipingana naye. Kufuatia upinzani huo, Sheikh Hussein Qummi alielekea Tehran kwa ajili ya mazungumzo na Shah.

Sheikh Abbas Qummi

 

Lakini baada ya kuingia tu katika bustani ya Shah alitiwa mbaroni na kuwekwa kizuizini sambamba na kuzuiwa kukutana na watu. Wananchi wa Mash’had wakiwa na lengo la kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa mwanazuoni huyo na wakati huo huo kuonyesha upinzani wao dhidi ya sera za mfalme huyo, walifanya mgomo wa kuketi katika Msikiti wa Goharshad kando ya Haram ya Imam Ridha (as). Vikosi vya usalama vilielekea katika msikiti huo na kufanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya watu waliokusanyika hapo, kiasi kwamba, takribani watu 1600 wasio na hatua waliuawa. Baada ya tukio hilo Sheikh Abbas Qummi aliondoka Mash’had na kuelekea Najaf na kuishi huko hadi mwishoni mwa umri wake.

Sheikh Abbas Qummi alikuwa alimu na msomi aliyekuwa akiifanyia kazi elimu yake. Kulipa umuhimu suala la elimu na amali, hatua kwa hatua kulimfanya Sheikh Abbas Qummi aondokee kuwa mashuhuri kama mmoja wa walezi wakubwa na walimu wa maadili (akhlaq) ya Kiislamu.

 

 

Sheikh Abbas Qummi alikuwa na shauku na mapenzi makubwa mno na kuandika na kusoma vitabu, hivyo mara nyingi alikuwa maktaba. Ni mara chache sana alionekana kutojishughulisha na kusoma na kukagua kitabu. Hata aliposafiri kwenda nchi za mbali kwa ajili ya ziyara alitumia muda wake wa faragha akiwa na vitabu.  Hakuna kitu ambacho kingeweza kupunguza huba, shauku na mapenzi yake ya kusoma na kuandika au kuwa kizuizi kwake katika njia hii.

 

Mwenyewe anasema: "Nilipokuwa nasoma Qom, nilikuwa maskini sana na kuna wakati nilikuwa nikidunduliza vijisenti na kufanikiwa kupata tumani (jina la sarafu ya Iran) 3." Nilikuwa nikichukua tomani hizo na kutembea kwa miguu kutoka Qom hadi Tehran, kwa ajili ya kwenda kutumia tomani hizo kwa ajili ya kununua nazo kitabu na kurudi Qom na kuendelea na masomo." Inaelezwa kuwa, kutabahari na kubobea kwake katika elimu na maarifa, katu hakukumfanya awe na majivuno na maringo. Kwa upande wa uandishi kama tulivyotangulia kusema, msomi huyu ndiye mwandishi wa kitabu mashuhuri cha dua cha Mafatihul-Jinan.

Kitabu hiki kina majimui na mkusanyiko wa dua mbalimbali, ziara, minong’ono na maelezo ya amali na matendo makhsusi ya ibada ya siku za mwaka pamoja na ada na adabu mbalimnbali zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (saww) na Maimamu watoharifu (as) pamopja na Maulamaa kuuhusiana na masuala mbalimbali ya kiibada. Kitabu cha Mafatihul Jinal kilichapishwa na kusambazwa mwaka 1925 mjini Mash’had na baada ya muda mfupi tu tangu kuenezwa kwake kikaondokea kupendwa na kupata umashuhuri mkubwa miongoni mwa waumini. Vitabu vingine vya mwanazuoni huyu ni Muntaha al-A’mal ambacho kinafafanua na kueleza historia ya Maasumina Kumi na Nne (as).

Sheikh Abbas Qummi hatimaye aliaga dunia 1940 baada ya kuishi maisha yaliyojaa uchajimungu na huduma kwa maarifa ya dini, na kuzikwa katika Haram ya Imam Ali (as) mjini Najaf jirani na kaburi la mwalimu wake marhumu muhaddith Nuri.

 

Wapenzi wasikilizaji kwa leo nakomea hapa. Msisite kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu. Hadi tutakapokutana tena juma lijalo ninakuageni nikiwa na matumaini ya kukutana nanyi wiki ijayo kwa tawfiq na mapenzi ya Mola Karima.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh