Aug 29, 2023 09:19 UTC
  • Iran inashikilia nafasi ya nne duniani katika makala za sayansi

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Iran imenyakua nafasi ya nne duniani katika mchango wa makala za kisayansi zinazohusiana na nanoteknolojia.

Idadi ya makala za Iran ambazo zilikuwa zimeorodheshwa katika Wavuti wa Sayansi (WoS)  ambayo ni hifadhidata kongwe zaidi, inayotumiwa sana na yenye mamlaka ya machapisho ya utafiti na manukuu , ilikuwa makala nane pekee mnamo 2000.  Baada ya kuanzishwa  Baraza la Ubunifu la Nanoteknolojia la Iran hali hiyo imebadilika.

Hadi kufikia mwaka 2022, wanasayansi wa Iran walikuwa na makala  11,473 katika WoS  na hivyo kuifanya Jamhuri ya Kiislamu kuwa mchangiaji mkubwa wa nne wa makala hizo katika kiwango cha kimataifa.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 4.9 ya makala zote za teknolojia ya nano ambazo zimechangiwa na watafiti wa kimataifa katika machapisho ya kisayansi mwaka 2022 na asilimia 8.25 ya idadi nzima ya makala za kisayansi zilizochangiwa na watafiti wa Iran kwenye WoS.

Miongoni mwa makala hizo, data zinaonyesha, asilimia 32 zilitayarishwa kwa pamoja kati ya watafiti wa Iran na watafiti kutoka nchi nyingine, hasa China, Marekani, Uturuki, Iraq na Kanada.

Kufikia mwisho wa 2022, wanasayansi wa Iran pia walisajili jumla ya uvumbuzi 312 katika ofisi za hataza zilizo Marekani na Ulaya. Idadi hiyo ni sawa na hataza 0.3 kwa kila makala 100 na pia inajumuisha asilimia 31 ya hataza zote zilizosajiliwa na vituo vya hataza vya Marekani na Ulaya.

Hatimaye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametimiza ahadi yake ya kuunda Bodi ya Umoja wa Mataifa ya Ushauri wa Kisayansi wakati huu ambapo teknolojia ya Akili Mnemba au au Akili Bandia ambayo kwa Kiingereza inajulikana kama ‘Artificial Intelligence’ (AI) imeshaanza kugonganisha vichwa vya watu kuhusu nafasi yake katika maendeleo duniani. 

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Guterres Bodi hii mpya aliyoiunda ni kwa ajili ya kuwashauri viongozi wa Umoja wa Mataifa kuhusu mafanikio katika sayansi na teknolojia na jinsi ya kutumia manufaa ya maendeleo haya na kupunguza hatari zinazoweza kutokea. 

Guterres anaamini maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia yanaweza kuunga mkono juhudi za kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu  lakini pia yanaleta wasiwasi wa kimaadili, kisheria na kisiasa, wasiwasi ambao unahitaji ufumbuzi wa kimataifa.  

Bodi ya Umoja wa Mataifa ya Ushauri wa Kisayansi ambayo Bwana Guterres anaamini pia kuwa itaimarisha jukumu la Umoja wa Mataifa kama chanzo cha kuaminika cha data na ushahidi wa kisayansi itajumuisha kundi la Maprofesa wanasayansi saba mashuhuri duniani. Maprofesa hao ni Profesa Yoshua Bengio, Profesa Sandra Díaz, Profesa Saleemul Huq, Profesa Fei-Fei Li, Profesa Alan Lightman, Profesa Thuli Madonsela, na Profesa Thomas C. Südhof. Pia kundi jingine ni Wanasayansi Wakuu wa mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa, na Mjumbe wa Katibu Mkuu kuhusu Teknolojia. 

Kupitia juhudi zao za ushirikiano, Bodi na Mtandao wake utawaunga mkono viongozi wa Umoja wa Mataifa katika kuelelewa maendeleo ya hivi karibuni ya kisayansi katika kazi yao kwa watu, sayari ya dunia na ustawi. 

Bodi hii itafanya kazi kama kitovu cha mtandao wa mitandao ya kisayansi. Lengo ni kuwa na muunganiko bora kati ya jumuiya ya kisayansi na kufanya uamuzi katika Umoja wa Mataifa. 

Ikumbukwe mwezi Julai mwaka huu, kwa mara ya kwanza Baraza la Usalama lilikuwa na mjadala mahususi kuhusu Akili Mnemba na mstakabali wake katika amani na usalama duniani na kabla yake, Katibu Mkuu Antonio Guterres kupitia moja ya matamko yake ya kisera ya Ajenda Yetu ya Pamoja, alitoa ahadi ambayo imetimia kwa kuunda Bodi hii ya kumshauri katika masuala ya kisayansi.

Ikumbukwe kuwa, Mwezi Julai, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikuwa na mjadala wa wazi kuhusu amani na usalama duniani likimulika fursa na hatari zitokanazo na Akili Mnemba au Akili Bandia, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisihi Baraza hilo lioneshe uongozi katika nyanja hiyo hasa katika kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika kujenga madaraja ya kijamii, kidijitali na kiuchumi badala ya kuleta utengano na uharibifu.

Na nchini Kenya WANASAYANSI na watafiti katika masuala ya kilimo wameibua hofu kuhusu matumizi kupita kiasi ya kemikali katika mimea.

Kilimo cha mahindi ndicho kinaongoza kwa matumizi ya kemikali kukabiliana na kero ya wadudu na magonjwa.

Dkt James Karanja, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (KALRO) tawi la Kabete alionya kwamba taifa lisipokuwa makini huenda suala hilo likawa janga.

Akizungumza hivi karibuni Jijini Nairobi, pia lilileta pamoja Wanasayansi wanaohamasisha kuhusu mifumo ya Bayoteknolojia kuboresha shughuli za kilimo na kudhibiti bidhaa.

Dkt Karanja ambaye ni mtaalamu wa uzalishaji mahindi na mtafiti mkuu katika mpango wa TELA (ushirikiano wa sekta ya umma na kibinafsi kutafiti bridi bora ya mahindi), alisema kwa sasa ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita, kiwango cha kemikali kinachotumiwa shambani kimepanda maradufu.

Huku wengi wakiendeleza dhana kuwa chakula kilichozalishwa kupitia ubunifu wa Bayoteknolojia hususan mazao ya GMO ndicho huchangia Saratani, Dkt Karanja asema kemikali katika kilimo ndizo kiini kikuu.