Jumatano, Juni 29, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 23 Ramadhani 1437 Hijria inayosadifiana na Juni 29, 2016.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita muungano wa visiwa vya Ushelisheli ulipata uhuru na kila inapowadia siku kama ya leo husherehekewa nchini humo kama siku ya taifa. Hadi kufikia katikati ya karne ya 18 wakati Wareno walipokuwa wakividhibiti visiwa hivyo, visiwa vingi vya Ushelisheli vilikuwa bado havijagunduliwa na watu hawakuwa wakiishi humo. Mapambano ya kupigania uhuru ya wazalendo wa visiwa vya Ushelisheli yalishika kasi tangu mwaka 1960 na miaka 16 baadaye Ushelisheli ikapata uhuru wake. Ushelisheli inaundwa na visiwa kadhaa ikipatikana mashariki mwa Afrika katika bahari ya Hindi huku jirani yake wa karibu zaidi kikiwa ni kisiwa cha Madagascar.
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita yaani tarehe 23 Ramadhani mwaka 1392 Hujria Qamaria, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai mwanafalsafa, arifu na faqihi mkubwa wa Kiirani alikamilisha kazi ya uandishi wa tafsiri kubwa na ya aina yake ya Qur’ani ya al Mizan. Tafsiri hiyo ya Qur’ani ni moja kati ya tafsiri kubwa na makini sana za Qur’ani Tukufu na iliandikwa katika kipindi cha karibu miaka 20. Sifa kubwa zaidi ya tafsiri hiyo ni kwamba imefasiri aya za Qur’ani kwa msaada wa aya nyingine za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Tafsiri hiyo kubwa na adhimu iliandikwa la Allamah Tabatabai kwa lugha ya Kiarabu na hadi sasa imetarjumiwa kwa lugha mbalimbali kama Kifarsi, Kiingereza na Kihispania.
Na miaka 103 iliyopita katika siku kama ya leo vilianza vita vya pili vya Balkan kati ya Bulgaria na umoja wa nchi za Serbia, Ugiriki, Montenegro, Romania na utawala wa Othmania. Ugiriki na Montenegro ambazo zilikuwa chini ya dola la Othmania (Ottoman Empire) baadaye zilifanya uasi dhidi ya dola hilo na nchi hizo zikafanikiwa kupata uhuru kutokana na kudhoofika Waothmania. Kwa msingi huo karibu asilimia 80 ya nchi zilizokuwa chini ya himaya ya Othmania huko Ulaya zikatoka chini ya udhibiti wa dola hilo, hata hivyo nchi zilizoshinda katika vita vya kwanza vya Balkan hazikuweza kufikia makubaliano ya kugawana ardhi zilizozikomboa na sababu hiyo kupelekea kuanza vita vya pili vya Balkan.