Jumatatu, tarehe 18 Septemba, 2023
Leo ni Jumatatu tarehe Pili Rabiul Awwal 1445 Hijria sawa na tarehe 18 Septemba 2023.
Siku kama ya leo miaka 815 iliyopita, aliaga dunia Ibn Athir Jazari, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na mpokezi mkubwa wa hadithi.
Ibn Athir alizaliwa mwaka 555 Hijria huko Iraq na kujifunza taaluma mbalimbali. Alipata umashuhuri katika masuala ya lugha na fasihi ya Kiarabu.
Kitabu maarufu zaidi cha Ibn Athir ni al Kamil fi Tarikh. Kitabu kingine cha mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ni Usdul Ghabah Fi Ma'rifatis Sahabah ambacho kinaeleza wasifu wa masahaba 7500 wa Mtume Muhammad (saw).

Katika siku kama ya leo miaka 314 iliyopita, alizaliwa Samuel Johnson mwandishi wa drama, malenga na mwandishi wa visa wa Kiingereza.
Alianza shughuli zake za fasihi sambamba na ukosoaji wake katika taaluma hiyo. Baada ya muda mwanatamthilia huyo aliingia katika uga wa utunzi wa mashairi. Samuel Johnson aliaga dunia mwaka 1784.

Katika siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, nchi ya Chile ilipata uhuru. Mwaka 1536 Chile ilidhibitiwa na Hispania. Sehemu kubwa ya kukoloniwa Chile, nchi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Naibu Mfalme wa Uhispania nchini Peru.

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita yaani tarehe 18 Septemba 1947, Shirika la Ujasusi la Marekani CIA lilianzishwa.
CIA ni miongoni mwa mashirika ya kijasusi ya kutisha sana duniani, na lina jukumu la kukusanya na kuchambua taarifa kuhusu serikali za nchi za kigeni, makampuni na watu binafsi na kuripoti taarifa hizo kwa serikali ya Marekani.
Shirika hili lilichukua nafasi ya Idara ya Huduma za Kimkakati, ambayo iliundwa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ili kuratibu shughuli za kijasusi kati ya matawi mbalimbali ya jeshi la Merekani.
Shirika la CIA, lenye idara na taasisi nyingi na pana, kama wakala wa ujasusi wa serikali ya Marekani, huwasaidia viongozi wa nchi hiyo katika kuingilia masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi ya nchi zingine.
Hadi sasa shirika hilo limehusika na mapinduzi ya serikali katika nchi mbalimbali zinazojitawala. Miongoni mwa mapinduzi hayo ni yale ya tarehe 28 Mordad 1332 Hijria Shamsia (19 Agosti 1953) nchini Iran kwa kushirikiana na shirika la ujasusi la Uingereza MI6.
Baada ya tukio la Septemba 11, 2001 lililoharibu majengo pacha (Twin Towers) huko New York, CIA ilipewa jukumu rasmi na la wazi la kuwateka nyara au kuwaua wapinzani wa Marekani duniani kote.

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita yaani tarehe 18 Septemba mwaka 1961 aliaga dunia Dag Hammarskjold mwanasiasa na Katibu Mkuu wa Pili wa Umoja wa Mataifa.
Mwanasiasa huyo wa nchini Sweden alifariki dunia baada ya ndege iliyokuwa imembeba wakati wa safari yake katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanguka.
Hammarskjold alikuwa Congo kwa lengo la kufanya mazungumzo na pande husika ili kumaliza vita vya ndani nchini humo. Mwanasiasa huyo alizaliwa mwaka 1905 na alihesabiwa katika zama zake kuwa mmoja kati ya waandishi stadi nchini Sweden. Mwaka 1952, Dag Hammarskjold alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobeli kutokana na harakati zake za kuimarisha amani duniani.

Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 27 Shahrivar mwaka 1367 Hijria Shamsia, aliaga dunia, Ustadh Muhammad Hussein Shahriyar mshairi mashuhuri wa Kiirani.
Alizaliwa mjini Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran na baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari katika Chuo cha Dar al-Funun mjini Tehran alijiunga na chuo cha tiba. Hata hivyo baada ya miaka michache aliacha masomo na kurejea katika kijiji alichozaliwa.
Ustadh Shahariyar alitoa mashairi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 23. Sambamba na kushadidi harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini, Shahriyar aliungana na wimbi hilo kwa kutumia mashairi yake.
Vilevile alikuwa mashuhuri sana kwa kumpenda Mtume wa Ahlubaiti zake na mapenzi hayo yalidhihiri katika tungo na mashairi yake.
