Alkhamisi 30 Juni, 2016
Leo ni Alkhamisi tarehe 24 Ramadhani 1437 Hijria inayosadifiana na Juni 30, 2016.
Miaka 27 iliyopita katika siku kama ya leo Jenerali Omar Hassan Ahmad al Bashir aliipindua serikali ya Sadiq al Mahdi iliyokuwa ikikabiliwa na migogoro ya ndani, katika mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu. Omar al Bashir na Dakta Hassan Turabi waliunda chama cha Congres ya Kitaifa ya Sudan kabla ya mapinduzi hayo na wao ndio waliokuwa wakiongoza chama hicho na kushikilia madaraka ya nchi.
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita mfumo wa ubaguzi wa rangi ulihitimishwa rasmi huko Afrika Kusini. Wazungu walio wachache wa Afrika Kusini waliwatwisha raia weusi wa nchi hiyo utawala wa ubaguzi wa rangi yaani Apartheid tangu mwaka 1948 na kwa mujibu wa mfumo huo wa kibaguzi, asilimia 20 ya wazungu wachache wa Afrika Kusini walitambulika kama watu wa tabaka la juu na wenye madaraka ya kuainisha mustakbali na kuongoza nchi. Aidha ndoa kati ya raia weusi na wazungu zilipigwa marufuku huko Afrika Kusini na wazalendo walizuiwa kuendesha shughuli za kisiasa.
Miaka 56 iliyopita mwafaka na tarehe 30 mwezi Juni 1960, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yaani Zaire ya zamani, ilitangaza uhuru wake. Kasavubu alichaguliwa kuwa Rais na Patrice Lumumba Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Kabla ya uhuru, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikuwa ikikoloniwa na Wabelgiji. Mapambano ya wapigania ukombozi wa Kongo chini ya uongozi wa mpigania uhuru mashuhuri wa Kiafrika Patrice Lumumba yalifikia kilele miaka kadhaa baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kupelekea kukombolewa Zaire ya zamani. Hata hivyo baada ya nchi hiyo kupata uhuru wake, serikali ya Ubelgiji ilihusika pakubwa katika kuzusha uasi mkubwa nchini humo. Aidha ulijiri mzozo kati ya Lumumba na Moise Tshombe kibaraka aliyekuwa na uhusiano wa wakoloni wa Kibelgiji na hivyo kuzidisha hali ya machafuko huko Zaire ya zamani. Nchi hiyo ilizidi kuwategemea wageni baada ya kuuawa Lumumba na vibaraka wa ndani. Hatimaye Jenerali Mobutu Seseseko alichukua madaraka katika mapinduzi ya mwaka 1965 Miladia kwa uungaji mkono wa Marekani na kuanza kuwakandamiza wananchi wa nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 727 iliyopita alifariki dunia Qutbuddin Shirazi, tabibu, mwanahesabati, mwanafikizia na mwanafalsafa wa Kiirani katika mji wa Tabrizi huko kaskazini magharibi mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi. Alibobea pia katika elimu za mantiki na irfani. Alifanya hima kubwa kutafuta elimu ya tiba na alihudumu kwa miaka mingi kama tabibu katika hospitali ya Shiraz, kusini mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa mtu wa kwanza kufanya uchunguzi kuhusu upinde wa mvua na kupata tafsiri ya kisayansi kuhusu suala hilo. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika taaluma mbalimbali.