Oct 02, 2023 02:27 UTC
  • Jumatatu, tarehe Pili Oktoba, 2023

Leo ni Jumatatu tarehe 16 Mfunguo Sita Rabiu Awwal 1445 Hijria mwafaka na tarehe Pili oktoba 2023.

Siku kama ya leo miaka 1444 kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Swala ya kwanza ya Ijumaa iliswaliwa na Mtume Muhammad (saw) baada ya mtukufu huyo kuhama mji wa Makka. Baada ya kuwasili katika eneo la Bani Salim bin Auf kwa jina la Quba karibu na Madina wakati wa adhuhuri, Mtume (saw) alitoa hotuba na kusimamisha Swala ya Ijumaa mahala hapo. Wanahistoria wanasema hiyo ilikuwa Swala ya kwanza ya Ijumaa katika Uislamu. Hatua hiyo pia inaonesha umuhimu wa ibada hiyo ya kiroho na kisiasa ambayo Bwana Mtume aliamua kuitekeleza mara tu baada ya kuwasili karibu na mji wa Madina. Baadaye Waislamu walijenga msikiti katika eneo hilo palipofanyika Swala ya Ijumaa ya kwanza katika Uislamu.

Siku kama ya leo miaka 836 iliyopita, mji wa Baitul-Muqaddas ulikombolewa na Salahuddin Ayyubi kamanda mwanamapambano wa Kiislamu. Awamu ya kwanza ya vita vya Msalaba  baina ya Wakristo na Waislamu vilianza 1096 ambapo miaka minne baadaye majeshi ya msalaba Mwekundu yalishambulia mji wa Baitul-Muqaddas na kuukalia kwa mabavu. Wanajeshi wao wa Msalaba walifanya uporaji na kuwauwa kikatili maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wasio na hatia wa ardhi hiyo. Hata hivyo mnamo mwaka 1187, baada ya Salahuddin Ayyubi kudhibiti Syria, Lebanon na Misri, aliuzingira mji wa Baitul-Muqaddas. Awali aliwatumia ujumbe wavamizi akiwaeleza heshima maalumu aliyonayo kwa mji huo na kutotaka kufanya umwagaji damu katika eneo hilo na kuwataka wavamizi hao waondoke katika mji huo na hata akawadhaminia usalama wa mali zao. Hata hivyo watu wa msalaba walikataa na hivyo kupelekea kuibuka vita na mji huo kukombolewwa na Waislamu katika siku kama ya leo wakiongozwa na kamanda Salahuddin Ayyubi.

Baitul Muqaddas

Miaka 154 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Mahatma Gandhi, kiongozi wa harakati ya kupigania uhuru nchini India katika moja ya vijiji vya jimbo la Gujarat. Mwaka 1891 Miladia Gandhi alirejea kutoka nchini Uingereza na kuishi mjini Mumbai. Mwaka 1893 Miladia Mahatma Gandhi alielekea mjini KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini. Akiwa nchini humo alishuhudia ubaguzi wa rangi wa jamii ya wachache ndani ya taifa hilo. Mwaka 1917 Miladia na baada ya kurejea nchini kwake alipata umashuhuri mkubwa. Na miaka michache baada ya Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia yaani akiwa na umri wa miaka 33 aliongoza mapambano kwa ajili ya kuwaokoa watu wake sanjari na kupigania uhuru wa India kutoka mikononi mwa Waingereza ambapo hatimaye na baada ya kuvumilia matatizo mengi akiwa na shakhsia tofauti kama vile Jawaharlal Nehru akafanikiwa kulipatia uhuru taifa hilo hapo mwaka 1947 Miladia. ***

Gandhi

Tarehe Pili Oktoba miaka 119 iliyopita alizaliwa Graham Greene mwandishi wa Uingereza. Mwandishi huyo aliakisi matendo mema na mabaya katika athari zake na aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa 'Nguvu na Utukufu' kwamba subira, uvumilivu na mateso ni njia ya wokovu. Graham Greene ameacha vitabu vingi na baadhi ni 'Mtu wa Tatu', 'Utawala Unaotisha' na Muuaji wa Kukodishwa'. Mwandishi huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1991.***

Graham Greene

Na katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita inayosadifiana na tarehe Pili Oktoba 1958, nchi ya Guinea Conakry ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno walianza kumiminika nchini Guinea mwishoni mwa karne ya 15, na mwanzoni mwa karne ya 19, Wafaransa walipata satua zaidi nchini humo. Mwaka 1849 nchi hiyo ilikoloniwa rasmi na Ufaransa. Guinea Conakry inapakana na nchi za Senegal, Mali, Ivory Coast, Liberia, Sierra Leone na Guinea Bissau.***

Bendera ya Guinea

 

Tags