Hikma za Nahjul Balagha (29)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 29 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine ya Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 29.
إِذَا کُنْتَ فِی إِدْبَارٍ وَ الْمَوْتُ فِی إِقْبَالٍ، فَمَا أَسْرَعَ الْمُلْتَقَى
Wakati maisha unayaacha nyuma kwa kasi na mauti yanakujia mbele yako kwa kasi, hiyo ni kasi kubwa kiasi gani mtu kukutana na mauti?
Tangu katika lahdha ya kwanza kabisa ya mtu kuzaliwa, kila saa inayopita katika maisha yake, huwa na maana ya kupungua sehemu ya mtaji wake wa kuishi hapa duniani. Kila pumzi anayovuta ni hatua moja mbele ya kukaribia zaidi kufikia mwisho wa maisha yake. Kwa sababu maisha ya mwanadamu hapa duniani yana mipaka na kuna siku yataisha tu. Ni kama vile taa, mwanga wa taa hiyo huendelea kupungua polepole na mwishowe huzima kabisa.
Harakati hii ya haraka inaendelea kila siku na kwa kila sekunde tahamaki muda wa mtu kuishi hapa duniani umeisha. Kuna na matukio mengine mbalimbali nayo husababisha vifo vya viumbe. Kuna matukio mbalimbali yakiwemo ya ajali, moto na magonjwa ambayo huhatarisha afya ya binadamu na kuwa sababu ya mtu kukutana haraka na kifo na kuondoka hapa duniani. Tunaweza kusema kuwa, mwendo wa kasi wa mwanadamu kuelekea mwishoni mwa maisha yake na nafasi ya matukio mbaslimbali ndani ya maisha ya mwanadamu, humharakisha mno kiumbe huyo kukutana na mauti. Ni sawa kabisa na vitu viwili vinavyokwenda kwa kasi kubwa mkabala wa kingine, hiki kinakijia hiki kwa kasi na hiki kingine nacho kinakijia hiki kwa kasi kubwa, bila ya shaka yoyote vitu hivyo viwili hukutana kwa haraka mno.
Katika Hikma hii ya 29 ya Nahjul Balagha Imam Ali AS anamuonya kila mtu kuhusu kasi hiyo ya kupindukia ya kuwasili dakika ya mwisho ya maisha ya mwanadamu. Imam hapa anasema: Wakati maisha unayaacha nyuma kwa kasi na mauti yanakujia mbele yako kwa kasi, hiyo ni kasi kubwa kiasi gani ya mtu kukutana na mauti?
Moja ya misingi mikuu ya kimalezi ya dini tukufu ya Kiislamu ambayo tunaipata katika mafundisho mengi ya dini hii tukufu ikiwemo kitabu cha Nahjul Balagha, ni kukumbushwa muda wote na kifo. Kifo si mwisho wa maisha, bali kifo ni mwisho wa safari ya mwanadamu katika marhala na hatua hii ya kupita kwa kasi na ya kupumbaza ya maisha ya duniani. Mtu ambaye ameghafilika na kifo chake huwa anaipapania mno dunia na hujidanganya kuwa ataishi milele hapa duniani. Ndio maana hajiandai kwa lolote katika kujiwekea akiba kwa ajili ya Akhera yake. Lakini kifo ni ukweli usiopingika. Mwenye busara kamwe huwa hawi msahaulifu. Mtu mwenye hikma muda wote hukumbuka kifo na huwa tayari amejiandaa kwa kuondoka duniani wakati wowote ule.
Imam Ali AS anatufundisha kuwa, njia bora kabisa ya kujiandaa kwa ajili ya kifo ni mtu muda wote kukumbuka kifo. Katika khutba ya 28 ya Nahjul Balagha mtukufu huyo anaashiria uchapwa wa dunia kwa kusema: Dunia inakupa mgongo na itakuacha mkono na hapo Akhera inakukabili na jeshi lake linakusubiri. Kuwa macho! Leo ni siku ya kufanyiwa mtihani na maandalizi na kesho ni siku ya mtihanani. Malipo ya watakaoshinda ni pepo na malipo ya waliobaki nyuma ni moto. Elewa! Mwenye kutenda mema kabla ya kifo chake, hujinufaisha mwenyewe na hatopata madhara baada ya kifo chake na anayeshindwa kuchukua hatua za maana kabla ya kifo chake, amepata hasara na kifo kitakuwa na madhara makubwa kwake.