Jul 01, 2016 00:10 UTC
  • Ijumaa, Julai 1, 2016

Leo ni Ijumaa tarehe 25 Ramadhani 1437 Hijria sawa tarehe Mosi Julai 2016.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, Imamu Mussa Sadr, mwanazuoni na msomi mashuhuri wa Lebanon alitoweka katika mazingira ya kutatanisha akiwa safarini nchini Libya. Alizaliwa mnamo mwaka 1928 katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baada ya kuhitimu masomo alielekea Lebanon. Baada ya kuwasili nchini humo, Imamu Mussa Sadr alichukua hatua kubwa za kuboresha maisha ya Walebanoni waliokuwa katika hali mbaya ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Mwanazuoni huyo pia alikuwa muungaji mkono wa harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina na aliasisi Harakati ya Wanyonge kwa ajili ya kutetea haki za Waislamu wa Lebanon. Hadi sasa juhudi mbalimbali za kutaka kujua hatima ya Imamu Mussa Sadr bado hazijazaa matunda.

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, nchi ndogo ya Burundi iliyoko barani Afrika ilitangaza kuwa huru. Nchi hiyo ilihesabiwa kuwa koloni la Ujerumani huko mashariki mwa Afrika katika miaka kati ya 1899 hadi 1917 Miladia sambamba na Rwanda. Jumuiya ya Mataifa iliikabidhi Ubelgiji mamlaka ya kuiongoza Burundi baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kushindwa Ujerumani. Aidha mwaka 1946, Umoja wa Mataifa ukatambua rasmi uongozi huo wa Ubelgiji nchini Burundi. Burundi ilijikomboa na kuasisi mfumo wa kifalme mwaka 1962. Hata hivyo miaka minne baadae Warepublikani wa nchi hiyo walimuondoa madarakani mfalme na kuasisi mfumo wa jamhuri. Burundi ina ukubwa wa kilomita mraba elfu 28 mashariki mwa bara la Afrika huku ikipakana na Rwanda, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo nchi iliyojulikana kwa jina la Somalia iliundwa na kujikomboa baada ya kuungana Somalia ya Uingereza na ya Italia. Mwaka 1884 sehemu ya ardhi ya Somalia ilikuwa chini ya mamlaka ya Uingereza na miaka mitano baadae Italia pia ikatwaa sehemu nyingine ya ardhi ya Somalia na kuikoloni. Mapambano yaliyoongozwa na Muhamad bin Abdallah Hassan dhidi ya Waingereza tangu mwaka 1901 hadi 1920 hayakufika popote. Na Hatimaye mwaka 1960 Somalia ya Italia na ya Uingereza zikapata uhuru wake na Jamhuri ya Somalia ikaundwa mnamo tarehe Mosi mwezi Julai mwaka huo. Somalia iko mashariki mwa bara la Afrika na kando ya bahari ya Hindi na Ghuba ya Aden. Aidha inapakana na Kenya, Ethiopia na Djibouti.

Tarehe Mosi Julai 1962 Rwanda nchi nyingine ndogo ya Kiafrika ilipata uhuru sambamba na Burundi. Rwanda ina historia inayoshabihiana na ya jirani yake kwa upande wa kusini yaani Burundi. Kabla ya kuwa huru, Rwanda ilikuwa ikikoloniwa na Ubelgiji. Rwanda ilipata uhuru mwaka 1962 Miladia mapambano ya ukombozi ya wapigania uhuru wa nchi hiyo. Kabila la Wahutu wa Rwanda linalotambuliwa kuwa kubwa zaidi nchini humo, ndilo lililoshika hatamu za uongozi baada ya nchi hiyo kupata uhuru. Jenerali Habyarimana alichukua madarakani ya nchi mwaka 1973 katika mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu. Hata hivyo katika mauaji ya kimbari yaliyojiri huko Rwanda mwaka 1994, Wahutu wenye misimamo mikali waliwauwa Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani zaidi ya laki nane kufuatia kutunguliwa ndege iliyokuwa imembeba Rais Juvenari Habyarimana. Watutsi walishika hatamu za uongozi baada ya kumalizika vita nchini humo mwaka 1994. Rwanda inapakana na Burundi, Uganda, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa na ukubwa wa kilomita mraba elfu ishirini na sita.  

Siku kama ya leo miaka 893 iliyopita alizaliwa Fakhrur Razi, khatibu, msomi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiislamu katika mji wa Rei ulioko kandokando ya jiji la Tehran. Khatibu Razi alibobea katika elimu nyingi za wakati huo na alifanya uhakiki na uchunguzi kuhusu masuala mbalimbali. Fakhr Razi alikuwa pia kinara wa elimu ya teolojia ya Kiislamu katika zama zake na aliandika vitabu vingi akikosoa maandishi na fikra za wasomi wa wakati huo.

Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ni kama Al Tibb al Kabiir, Asrarut Tanzil na Mafatihul Ghaib. Vilevile aliandika tabu kubwa la maarifa ya Kiislamu (Encyclopedia) ambalo alilipa jina la Jamiul Uluum.