Jul 02, 2016 01:35 UTC
  • Jumamosi, Julai Pili, 2016

Leo ni Jumamosi tarehe 26 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka 1437 Hijria mwafaka na tarehe Pili Julai mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita alizaliwa Patrice Lumumba muasisi wa uhuru wa Kongo. Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa. Lumumba aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokita "Congo, My Country yaani Kongo, Nchi Yangu." ***

Katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, ndege moja ya abiria aina ya Airbus ya Iran ilitunguliwa kwa makombora mawili ikiwa juu ya anga ya maji ya Ghuba ya Uajemi ikitokea Bandar Abbas kusini mwa Iran kuelekea Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Makombora hayo yalirushwa kutoka kwenye meli za kivita za Marekani katika maji ya Ghuba ya Uajemi. Abiria wote 298 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo wakiwemo watoto 66 waliuawa katika shambulizi hilo la kichokozi. Jinai hiyo ilionesha kiburi na dharau ya Marekani na jinsi nchi hiyo inavyopuuza sheria zote za kimataifa na maazimio ya kutetea haki za binadamu na kuamua kutungua hata ndege ya abiria. *** 

Miaka 55 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway. Alizaliwa mwaka 1899 na kwa muda fulani alikuwa mwanahabari huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway ndiye aliyebuni uandishi wa visa vifupi vifupi kwa kutumia lugha nyepesi. Mwaka 1954 Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi. Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na For Whom The Bell Tolls". ***

Katika siku kama ya leo miaka 127 iliyopita, mfumo wa kisultani ulifutwa huko Brazil na badala yake ukaasisiwa mfumo wa jamhuri bila ya umwagaji damu wowote na katika hali ya utulivu. Mfalme wa mwisho wa Brazil alikuwa Pedro II  ambaye alifanya jitihada za kufanya mabadiliko nchini humo. Hatua za mfalme huyo hususan ile ya kuondoa biashara ya utumwa mwaka 1888, iliwakasirisha wamiliki wa ardhi waliokuwa wakiunga mkono mfumo wake wa kisultani. Pedro II alienguliwa madarakani bila ya mapambano yoyote na mfumo wa jamhuri ukaasisiwa nchini Brazil. ***

Na siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, Allama Abdul Hussein Amini alimu na fakihi mkubwa wa Kiislamu ambaye pie ndiye mwandishi wa kitabu chenye thamani kubwa cha al-Ghadir alifariki dunia. Alizaliwa katika mji wa Tabriz nchini Iran na kukipitisha kipindi cha utoto wake katika familia ya kidini na chini ya usimamizi wa baba yake aliyekuwa mmoja wa maulama mashuhuri katika zama hizo.***